Agano la Kale

Agano Jipya

Waamuzi 9:22-39 Biblia Habari Njema (BHN)

22. Abimeleki alitawala juu ya Israeli kwa muda wa miaka mitatu.

23. Kisha Mungu akaleta roho ya uadui kati ya Abimeleki na watu wa Shekemu, nao wakamwasi.

24. Ndivyo walivyoadhibiwa watu wa Shekemu pamoja na ndugu yao Abimeleki kwa ukatili waliowafanyia wana sabini wa Yerubaali. Adhabu ya mauaji hayo iliwapata maana Abimeleki aliwaua akisaidiwa na hao watu wa Shekemu.

25. Watu wa Shekemu waliweka washambulizi wamwotee Abimeleki kutoka vilele vya mlima. Watu hao waliwanyanganya mali zao wote waliopita huko. Abimeleki akaambiwa mambo hayo.

26. Siku moja Gaali, mwana wa Ebedi, pamoja na ndugu zake alikwenda kukaa Shekemu. Watu wa Shekemu wakawa na imani naye.

27. Wakatoka na kwenda kwenye mashamba yao ya mizabibu, wakachuma zabibu halafu wakazisindika, wakatengeneza divai wakafanya sikukuu. Wakaingia kwenye nyumba ya mungu wao wakala na kunywa; kisha wakamtukana Abimeleki.

28. Gaali, mwana wa Ebedi, akasema, “Abimeleki ni nani? Sisi hapa Shekemu ni watu wa aina gani hata tumtumikie Abimeleki? Gideoni na Zebuli ofisa wake walimtumikia Hamori baba wa Shekemu, lakini kwa nini basi, sisi tumtumikie Abimeleki?

29. Kama watu hawa wangekuwa chini yangu, ningemwondoa Abimeleki. Ningemwambia Abimeleki, ‘Ongeza jeshi lako, kisha, njoo hadharani tupigane.’”

30. Zebuluni, mtawala wa mji, aliposikia maneno ya Gaali mwana wa Ebedi, alikasirika sana.

31. Basi akampelekea ujumbe Abimeleki huko Torma akasema, “Gaali, mwana wa Ebedi, pamoja na ndugu zake wameingia mjini Shekemu na kuchochea uasi dhidi yako.

32. Basi, rudi wewe na watu ulio nao, wakati wa usiku, uvizie mashambani karibu na mji.

33. Mara jua litakapotoka wakati wa asubuhi, ushambulie mji. Gaali akitoka pamoja na watu wake kuja kukukabili, uwatendee ifaavyo.”

34. Abimeleki aliondoka na watu waliokuwa pamoja naye kuja Shekemu wakati wa usiku. Aliwagawa watu wake katika vikosi vinne na kuvizia huko karibu na mji.

35. Gaali, mwana wa Ebedi, akatoka nje na kusimama kwenye lango la mji, wakati huo Abimeleki na watu wake walitoka mahali walipokuwa wanavizia.

36. Gaali alipomwona akamwambia Zebuli, “Tazama, watu wanashuka kutoka vilele vya mlima.” Zebuli akamwambia, “Wewe unaona vivuli vya milima kana kwamba ni watu.”

37. Gaali akasema tena, “Tazama! Watu wanashuka katikati ya nchi na kikosi kingine kinatoka upande wa Mwaloni wa Waaguzi.”

38. Kisha Zebuli akamwambia, “Majivuno yako yako wapi sasa? Si ni wewe uliyesema, ‘Abimeleki ni nani? Kwa nini tumtumikie?’ Sasa, hao ndio watu uliowadharau; nenda ukapigane nao.”

39. Gaali akatoka akiwaongoza watu wa Shekemu na kupigana na Abimeleki.

Kusoma sura kamili Waamuzi 9