Agano la Kale

Agano Jipya

Waamuzi 9:14-30 Biblia Habari Njema (BHN)

14. Mwishowe miti yote ikauendea mti wa miiba na kuuambia, ‘Njoo wewe utawale juu yetu.’

15. Mti wa miiba ukajibu, ‘Kama kweli mnataka kuniteua kuwa mfalme, njoni mkae chini ya kivuli changu. Lakini kama hamtaki kufanya hivyo, basi moto na utoke kwenye miiba yangu na kuiteketeza hata mierezi ya Lebanoni.’”

16. Yothamu akaendelea kusema, “Sasa basi, mnadhani mmefanya Abimeleki mfalme kwa nia njema na uaminifu? Je, mnadhani mmemtendea wema Yerubaali na jamaa yake kama alivyostahili kwa matendo yake?

17. Aghalabu baba yangu alihatarisha maisha yake kwa kuwapigania na kuwakomboa kutoka kwa Wamidiani!

18. Lakini leo mmeishambulia jamaa ya baba yangu na kuwaua wana sabini juu ya jiwe moja, halafu mmemfanya Abimeleki mtoto wa mjakazi wa baba, awe mfalme wa wakazi wa Shekemu kwa sababu tu ni mtu wa ukoo wenu.

19. Sasa basi, kama mmetenda hayo kwa nia njema na kwa kumheshimu Yerubaali na jamaa yake, basi, furahini pamoja na Abimeleki, naye afurahi pamoja nanyi.

20. Lakini, kama sivyo, moto na utoke kwa Abimeleki na kuwateketeza wananchi wa Shekemu na Beth-milo, tena moto utoke kwa wananchi wa Shekemu na Beth-milo na kumteketeza Abimeleki.”

21. Kisha Yothamu akatoroka, akakimbilia Beeri, akakaa huko, kwa maana alimwogopa Abimeleki ndugu yake. Akakaa huko.

22. Abimeleki alitawala juu ya Israeli kwa muda wa miaka mitatu.

23. Kisha Mungu akaleta roho ya uadui kati ya Abimeleki na watu wa Shekemu, nao wakamwasi.

24. Ndivyo walivyoadhibiwa watu wa Shekemu pamoja na ndugu yao Abimeleki kwa ukatili waliowafanyia wana sabini wa Yerubaali. Adhabu ya mauaji hayo iliwapata maana Abimeleki aliwaua akisaidiwa na hao watu wa Shekemu.

25. Watu wa Shekemu waliweka washambulizi wamwotee Abimeleki kutoka vilele vya mlima. Watu hao waliwanyanganya mali zao wote waliopita huko. Abimeleki akaambiwa mambo hayo.

26. Siku moja Gaali, mwana wa Ebedi, pamoja na ndugu zake alikwenda kukaa Shekemu. Watu wa Shekemu wakawa na imani naye.

27. Wakatoka na kwenda kwenye mashamba yao ya mizabibu, wakachuma zabibu halafu wakazisindika, wakatengeneza divai wakafanya sikukuu. Wakaingia kwenye nyumba ya mungu wao wakala na kunywa; kisha wakamtukana Abimeleki.

28. Gaali, mwana wa Ebedi, akasema, “Abimeleki ni nani? Sisi hapa Shekemu ni watu wa aina gani hata tumtumikie Abimeleki? Gideoni na Zebuli ofisa wake walimtumikia Hamori baba wa Shekemu, lakini kwa nini basi, sisi tumtumikie Abimeleki?

29. Kama watu hawa wangekuwa chini yangu, ningemwondoa Abimeleki. Ningemwambia Abimeleki, ‘Ongeza jeshi lako, kisha, njoo hadharani tupigane.’”

30. Zebuluni, mtawala wa mji, aliposikia maneno ya Gaali mwana wa Ebedi, alikasirika sana.

Kusoma sura kamili Waamuzi 9