Agano la Kale

Agano Jipya

Waamuzi 8:14-22 Biblia Habari Njema (BHN)

14. Akamkamata kijana mmoja wa Sukothi na kumhoji. Kijana huyo akamwandikia majina ya viongozi na wazee mashuhuri wa Sukothi, jumla yao watu sabini na saba.

15. Gideoni akarudi kwa watu wa Sukothi, akawaambia, “Si mtakumbuka mlivyonitukana mliposema, ‘Kwa nini tuwape mikate watu wako waliochoka sana nanyi bado hamjamshinda Zeba na Salmuna?’ Haya basi, Zeba na Salmuna ndio hawa.”

16. Basi, akawachukua wazee wa Sukothi na kuwapa funzo wanaume wote kwa kuichana miili yao kwa miiba na mbigili.

17. Vilevile akaubomoa mnara wa Penueli na kuwaua wakazi wa mji huo.

18. Kisha, akawauliza Zeba na Salmuna, “Watu wale mliowaua huko Tabori walikuwaje?” Wakamjibu, “Walifanana na wewe, maana walionekana kama wana wa mfalme.”

19. Naye akawaambia, “Hao walikuwa ndugu zangu, wana wa mama yangu mzazi. Naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, kama msingewaua, hata mimi nisingewaua.”

20. Kisha akamwambia Yetheri, mzaliwa wake wa kwanza, “Simama, uwaue.” Lakini Yetheri aliogopa kuchukua upanga wake maana alikuwa bado kijana.

21. Hapo Zeba na Salmuna wakasema, “Tuue wewe mwenyewe, maana hii ni kazi ya mtu mzima.” Gideoni akawaua yeye mwenyewe na kuchukua mapambo yao yaliyokuwa shingoni mwa ngamia wao.

22. Kisha, Waisraeli wakamwambia Gideoni, “Wewe na uwe mtawala wetu, na baada yako watutawale wazawa wako, kwa kuwa wewe umetukomboa kutoka kwa Wamidiani.”

Kusoma sura kamili Waamuzi 8