Agano la Kale

Agano Jipya

Malaki 2:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Mwenyezi-Mungu wa majeshi awaambia makuhani: “Sasa enyi makuhani, nawaamuruni hivi:

2. Ni lazima mniheshimu mimi kwa matendo yenu, msiponisikiliza nitawaleteeni laana, vitu vyote mnavyopewa kwa mahitaji yenu nitavilaani. Na kweli nimekwisha kuvilaani, kwa sababu hamuyatilii maanani maagizo yangu.

3. Tazama, nitawaadhibu watoto wenu na nyinyi wenyewe kutokana na uovu wenu, na kuzipaka nyuso zenu mavi ya wanyama wenu wa tambiko. Nitawafukuza mbali nami.

4. Hivyo mtajua kuwa nimewapeni amri hii ili agano langu na ukoo wa Lawi liwe la kudumu.

5. “Katika agano hilo, niliwaahidi uhai na amani na kwamba wao ni lazima kunicha mimi, nao kwa upande wao walinicha mimi, wakaliogopa jina langu.

6. Mafundisho yao yalikuwa ya kweli na kamwe hawakufundisha uongo. Mimi na wao tulikaa kwa amani. Si kwamba walitenda haki tu, bali waliwafundisha wengine kutotenda maovu.

7. Ni wajibu wa makuhani kuwafundisha watu maarifa ya kweli juu ya Mungu. Watu wawaendee kujifunza matakwa yangu kwao, kwani makuhani ni wajumbe wa Mwenyezi-Mungu wa majeshi.

8. “Bali nyinyi makuhani mmegeuka mkaiacha njia ya haki. Mafundisho yenu yamewaongoza watu wengi katika kutenda mabaya. Mmelivunja agano nililofanya nanyi.

9. Nami pia nitawafanya mdharauliwe na kupuuzwa na Waisraeli, kwa sababu hamkuzifuata njia zangu, na mnapowafundisha watu wangu mnapendelea baadhi yao.”

10. Je, sisi sote si watoto wa baba mmoja? Je, sisi sote hatukuumbwa na Mungu yuleyule? Mbona basi, hatuaminiani sisi kwa sisi, na tunalidharau agano alilofanya Mwenyezi-Mungu na wazee wetu?

Kusoma sura kamili Malaki 2