Agano la Kale

Agano Jipya

Isaya 44:6-22 Biblia Habari Njema (BHN)

6. Mwenyezi-Mungu, Mfalme na Mkombozi wa Israeli,naam, Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi:“Mimi ni wa kwanza na wa mwisho;hakuna Mungu mwingine ila mimi.

7. Ni nani Mungu aliye kama mimi?Mwache atangaze na kusema wazi mbele yangu.Nani alitangaza hapo kale mambo ambayo yatatukia?Na watuambie yale ambayo bado kutokea.

8. Enyi watu wangu, msiogope wala msiwe na hofu,Je, sikuwaambia tangu zamani mambo yatakayotokea?Nyinyi ni mashahidi wangu.Je, yuko Mungu mwingine ila mimi?Je, kuna mwenye nguvu mwingine?Huyo simjui!”

9. Watu wote wanaotengeneza sanamu za miungu ni bure kabisa; na vitu hivyo wanavyovifurahia haviwafai chochote. Wanaoshuhudia hiyo miungu ya uongo ni vipofu na wajinga. Kwa hiyo hao wataaibishwa!

10. Ajabu ya mtu kutengeneza sanamu au kinyago cha mungu ambaye hawezi kumsaidia chochote!

11. Hakika wote wanaomheshimu wataaibishwa, tena hao mafundi wa sanamu ni binadamu tu. Basi, wakutane wote, wajitokeze, nao watatishika na kuaibishwa.

12. Mfuachuma huchukua madini, akayayeyusha motoni na kufua sanamu. Huigongagonga kwa nyundo ili kuipa umbo kwa mikono yake yenye nguvu. Wakati wote huo yeye huona njaa na kuchoka; huona kiu na nguvu kumwishia.

13. Kadhalika naye seremala hupima kipande cha mbao, akakitia alama kwa kalamu yake, kisha kwa vifaa vyake hukichonga na kukipa umbo la binadamu na sura ya kupendeza; kisha akaiweka sanamu hiyo ya mungu mahali pake pa pekee.

14. Mtu hukata mti wa mwerezi ili autumie, au huchagua mberoshi au mwaloni. Huuacha ukue kati ya miti ya msituni. Au hupanda mwerezi na mvua huustawisha.

15. Sehemu ya mti huo itatumiwa kama kuni; mtu huota moto wake na kuoka mikate yake juu yake. Sehemu nyingine ya mti huohuo, mtu hujichongea sanamu ya mungu, akainakshi, halafu akaiabudu.

16. Kisha huchukua kuni zake akaoka nazo moto, akachoma nyama juu yake, akala, akashiba. Halafu hukaa hapo akiota moto na kusema, “Naam! Ama kweli nimepata joto! Huo ndio moto!”

17. Sehemu iliyobaki ya mti huohuo, hujichongea sanamu ya mungu, kinyago chake, kisha huisujudia na kuiabudu. Huiomba akisema, “Wewe ni mungu wangu, niokoe!”

18. Watu hao hawajui wala hawaelewi kitu chochote. Wamefumbwa macho wasiweze kuona; kadhalika na akili zao wasiweze kufahamu.

19. Hakuna awezaye kutafakari; au kuwa na akili na kufikiri na kusema: “Nusu ya mti huo niliwashia moto; tena nikaoka mikate juu ya makaa yake, nikachoma nyama, nikala. Je, sehemu iliyobaki nitatengeneza sanamu ambayo ni chukizo na kukisujudia hicho kipande cha mti?”

20. La! Fikira zake zimeambatana na hicho ambacho ni majivu tu! Mtu huyo amepotoka hata hawezi kujiokoa mwenyewe na kusema: “Kweli ninachoshika mkononi ni udanganyifu mtupu!”

21. Mwenyezi-Mungu asema hivi:“Ewe taifa la Yakobo kumbuka;naam, kumbuka ewe Israeli:Wewe ni mtumishi wangu.Nilikuumba ili uwe mtumishi wangu,nami kamwe sitakusahau.

22. Nimeyafagilia mbali makosa yako kama wingu,nimezifanya dhambi zako zitoweke kama ukungu.Rudi kwangu maana mimi nimekukomboa.”

Kusoma sura kamili Isaya 44