Agano la Kale

Agano Jipya

Hesabu 35:12-29 Biblia Habari Njema (BHN)

12. Miji hiyo itakuwa mahali pa kukimbilia usalama ili huyo mwuaji asiuawe na mwenye kulipiza kisasi kabla ya kuhukumiwa na jumuiya.

13. Mtajitengea miji sita kwa ajili ya makimbilio.

14. Kati ya miji hiyo sita mtakayoitenga, mitatu iwe mashariki ya Yordani, na mitatu iwe katika nchi ya Kanaani.

15. Miji hii itakuwa ya makimbilio kwa ajili ya Waisraeli na wageni wa kudumu au wa muda wanaokaa pamoja nao. Mtu yeyote akimuua mwingine bila kukusudia anaweza kukimbilia huko.

16. “Lakini mtu akimpiga mwenzake kwa kitu cha chuma, akafa, mtu huyo ni mwuaji na ni lazima auawe.

17. Mtu yeyote akimpiga mwenzake kwa jiwe, akifa, mtu huyo ni mwuaji, na lazima auawe.

18. Kama akimpiga mwenzake kwa silaha ya mti ambayo yaweza kusababisha kifo, akafa, mtu huyo ni mwuaji, na ni lazima auawe.

19. Jamaa wa karibu wa mtu aliyeuawa atalipiza kisasi. Huyu atakapokutana na huyo mwuaji, atatekeleza hukumu ya kifo.

20. “Hali kadhalika, kama mtu anamchukia mwenzake halafu, akamsukuma au kumtupia kitu kwa kumvizia,

21. au kwa kumpiga ngumi akafa, basi mtu huyo aliyempiga mwenzake ni mwuaji na ni lazima auawe. Jamaa wa karibu wa mtu aliyeuawa atalipiza kisasi atakapokutana naye.

22. “Lakini kama mtu akimsukuma mwenzake kwa ghafla bila chuki au kumtupia kitu bila kumvizia

23. au mtu akirusha jiwe linaloweza kusababisha kifo, akamuua mtu bila kukusudia, ingawa hakuwa adui yake wala hakutaka kumdhuru,

24. basi, jumuiya itaamua kati ya huyo mwuaji na jamaa ya mtu aliyeuawa anayetaka kulipiza kisasi, kulingana na sheria hizi.

25. Jumuiya itamwokoa mtu huyo aliyeua mikononi mwa jamaa ya mtu aliyeuawa, na kumrudisha katika mji wa makimbilio alimokuwa amekimbilia. Atakaa huko mpaka kifo cha kuhani mkuu wa wakati huo aliyeteuliwa kwa kupakwa mafuta matakatifu.

26. Lakini huyo aliyeua akitoka nje ya mji aliokimbilia wakati wowote ule,

27. halafu jamaa ya mtu aliyeuawa akampata nje ya mipaka ya mji huo wa makimbilio akamuua, huyo hatakuwa na hatia ya kuua.

28. Maana huyo aliyeua ni lazima akae ndani ya mji wa makimbilio mpaka kuhani mkuu atakapofariki; lakini baada ya kifo cha kuhani mkuu anaweza kurudi nyumbani.

29. “Sheria hizi zitatumika katika vizazi vyenu vyote, mahali popote mtakapokaa.

Kusoma sura kamili Hesabu 35