Sura

  1. 1
  2. 2
  3. 3
  4. 4
  5. 5
  6. 6
  7. 7
  8. 8
  9. 9
  10. 10
  11. 11
  12. 12
  13. 13
  14. 14
  15. 15
  16. 16
  17. 17
  18. 18
  19. 19
  20. 20
  21. 21
  22. 22
  23. 23
  24. 24
  25. 25
  26. 26
  27. 27
  28. 28
  29. 29
  30. 30
  31. 31
  32. 32
  33. 33
  34. 34
  35. 35
  36. 36
  37. 37
  38. 38
  39. 39
  40. 40
  41. 41
  42. 42
  43. 43
  44. 44
  45. 45
  46. 46
  47. 47
  48. 48

Agano la Kale

Agano Jipya

Ezekieli 46 Biblia Habari Njema (BHN)

1. “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Lango la ua wa ndani unaoelekea mashariki litafungwa siku zote sita za kazi. Siku za sabato na siku za mwezi mwandamo litafunguliwa.

2. Toka nje, mtawala ataingia ukumbi wa ndani kwa kupitia lango la ukumbi huo. Naye atasimama karibu na nguzo ya lango, wakati makuhani wanateketeza sadaka zake za kuteketezwa na sadaka za amani. Kisha mtawala huyo atasujudia kwenye lango na baadaye atatoka nje. Lango litabaki wazi hadi jioni.

3. Kila siku ya sabato na sikukuu ya mwezi mwandamo, watu wote wataniabudu mimi Mwenyezi-Mungu mbele ya lango.

4. Siku ya sabato, mtawala atamletea Mwenyezi-Mungu wanakondoo sita na kondoo dume mmoja, wote wasio na dosari, kama sadaka ya kuteketezwa nzima.

5. Pamoja na kila kondoo dume, ataleta sadaka ya unga lita kumi na saba na nusu, lakini pamoja na kila mwanakondoo ataleta sadaka yoyote anayoweza. Na kwa kila sadaka ya unga, ataleta lita tatu za mafuta.

6. Wakati wa sikukuu ya mwezi mwandamo atatoa fahali mchanga, wanakondoo sita, na kondoo dume mmoja; wote wasio na dosari.

7. Pamoja na kila fahali na kila kondoo dume anayetolewa sadaka, ni lazima pawepo lita kumi na saba na nusu za unga, na pamoja na kila mwanakondoo, ni lazima pawepo chochote ambacho mtawala anatoa. Tena kwa kila sadaka ya nafaka, ni lazima kutoa lita tatu za nafaka.

8. “Mtawala anapotoka ni lazima auache ukumbi kwa njia ileile aliyoingia nayo.

9. Watu wanapokuja kumwabudu Mwenyezi-Mungu wakati wa sikukuu yoyote, wale walioingia kwa njia ya lango la kaskazini, watatoka kwa njia ya lango la kusini; na wale walioingia kwa lango la kusini, watatoka kwa njia ya lango la kaskazini. Mtu asirudi kwa njia ya lango aliloingilia, bali atatoka kwa njia ya lango lililo mbele yake.

10. Mtawala ataingia ndani watu wanapoingia, na atatoka wanapotoka.

11. Wakati wa siku za sikukuu na siku zilizopangwa, sadaka za nafaka zitakuwa lita kumi na saba zikiandamana na kila fahali au kondoo dume, na chochote ambacho anayeabudu anaweza kutoa kwa kila mwanakondoo. Kwa kila sadaka ya nafaka atatoa lita tatu za mafuta.

12. Mtawala anapotaka kumtolea Mwenyezi-Mungu sadaka kwa hiari, iwe sadaka ya kuteketezwa au sadaka ya amani, watamfungulia lango la ukumbi wa ndani unaoelekea mashariki. Atatoa sadaka kama anavyofanya siku ya sabato, na anapotoka, lango lifungwe nyuma yake.

Dhabihu za kila siku

13. “Kila siku asubuhi mtamtolea Mwenyezi-Mungu mwanakondoo wa mwaka mmoja asiye na dosari, ambaye atateketezwa mzima.

14. Pia kila siku, sadaka ya kilo mbili za unga itatolewa asubuhi pamoja na lita moja ya mafuta ya zeituni yakichanganywa na unga. Ni lazima kufuata sheria za sadaka hii kwa Mwenyezi-Mungu milele.

15. Mwanakondoo, unga na mafuta ni lazima vitolewe kila siku asubuhi kwa Mwenyezi-Mungu milele.

Mtawala na ardhi

16. “Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Ikiwa mtawala anampa mmojawapo wa wanawe zawadi ya ardhi, zawadi hiyo itakuwa mali ya huyo kijana milele kama sehemu ya jamaa yake.

17. Lakini ikiwa atampa mmoja wa watumishi wake sehemu yoyote ya ardhi yake, zawadi hiyo itakuwa mali yake mpaka mwaka wa kuachwa huru. Ndipo itakapomrudia mtawala. Ni yeye tu na watoto wake wa kiume wanaoweza kuimiliki daima.

18. Mtawala kamwe asipore mali ya watu. Ardhi yoyote anayowapa watoto wake wa kiume ni lazima itokane na eneo lake mwenyewe. Hivyo hatawadhulumu watu wangu kwa kuwanyanganya ardhi yao.”

Majiko ya hekalu

19. Kisha, yule mtu akanipitisha kwenye nafasi ya kupitia kuingia kwenye vyumba vitakatifu vya makuhani vinavyoelekea kaskazini, karibu na lango la kusini la ukumbi wa ndani. Akanionesha mahali, upande wa magharibi wa vyumba,

20. akaniambia: “Hapa makuhani huchemsha nyama ya sadaka ya kuondoa hatia, sadaka ya kuondoa dhambi, na kuoka sadaka za nafaka. Kwa hiyo hawatoki nje ya ukumbi na chochote, ili watu wasije wakawa najisi kwa kugusa kitu kitakatifu.”

21. Kisha akanipeleka kwenye uwanja wa nje, akanipitisha karibu na pembe nne za ua; kwa kila pembe ya ua kulikuwapo kiwanja kidogo,

22. yaani, kwa pembe nne za ua vilikuwapo viwanja vinne vidogo vya urefu wa mita 20 na upana mita 15.

23. Ulikuwapo ukuta kukizunguka kila kiwanja, na mahali pa moto mkabala na ukuta.

24. Yule mtu akaniambia: “Haya ni majiko ambako watumishi wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu watachemsha sadaka wanazoleta watu.”