Agano la Kale

Agano Jipya

Ezekieli 33:5-19 Biblia Habari Njema (BHN)

5. Aliisikia sauti ya tarumbeta, akapuuza onyo; basi lawama ya kifo chake itakuwa juu yake mwenyewe. Lakini kama angejali hilo onyo, angeyaokoa maisha yake.

6. “Lakini kama yule mlinzi akiona adui wanakuja asipige tarumbeta na watu wakawa hawakuonywa juu ya hatari inayokuja, maadui wakaja na kumuua mtu yeyote miongoni mwao; huyo mtu aliyekufa, atakuwa amekufa kwa kosa lake. Lakini mimi nitamdai mlinzi kifo cha mtu huyo.

7. “Basi, ewe mtu, nimekuweka kuwa mlinzi wa Waisraeli. Utakaposikia neno kutoka kwangu utawapa onyo langu.

8. Nikimwambia mtu mwovu: ‘Wewe mtu mwovu hakika utakufa’; lakini wewe husemi chochote ili kumwonya yule mtu mwovu aachane na mwenendo wake; mtu huyo hakika atakufa kwa kosa lake; walakini nitakudai wewe kifo chake.

9. Lakini ukimwonya mwovu aachane na mwenendo wake, naye haachani na mwenendo wake mbaya, yeye atakufa kwa kosa lake; lakini wewe utakuwa umeyaokoa maisha yako.

10. “Ewe mtu! Waambie Waisraeli jambo hili: Nyinyi mwasema, ‘Tumezidiwa na makosa na dhambi zetu. Tunadhoofika kwa sababu yake! Tutawezaje basi, kuishi?’

11. Basi, waambie: Kama niishivyo mimi Bwana Mwenyezi-Mungu naapa kwamba, mimi sikifurahii kifo cha mtu mwovu, bali napenda mtu mwovu aachane na mwenendo wake mbaya, apate kuishi. Tubuni, achaneni na mwenendo wenu mbaya, enyi Waisraeli! Kwa nini mwataka kufa?

12. “Basi, ewe mtu, waambie wananchi wenzako hivi: Mtu mwadilifu akitenda uovu, uadilifu wake hautamwokoa. Na mtu mwovu akiacha kutenda dhambi hataadhibiwa. Mtu mwadilifu akianza kutenda dhambi uadilifu wake hautamsalimisha.

13. Mimi namwahidi mwadilifu kwamba ataishi; lakini yeye akiamini kwamba uadilifu wake watosha, akaanza kutenda uovu, matendo yake yote mema ya hapo awali hayatakumbukwa; atakufa kwa uovu wake.

14. Tena, nikimwambia mtu mwovu kuwa hakika atakufa naye akaiacha dhambi yake, akaanza kutenda yaliyo ya haki na sawa, hatakufa;

15. kama akirudisha rehani na kurudisha alichoiba, akafuata kanuni ziletazo uhai bila kutenda uovu, mtu huyo hakika ataishi; hatakufa.

16. Dhambi zake zote alizotenda hapo awali hazitakumbukwa; yeye ametenda yaliyo ya haki na mema; kwa hiyo hakika ataishi.

17. “Lakini wananchi wenzako wasema ati: ‘Anachofanya Mwenyezi-Mungu si sawa!’ Kumbe kwa kweli wao ndio hawafanyi kilicho sawa.

18. Mtu mwadilifu akiacha uadilifu wake, akaanza kutenda uovu, atakufa kwa sababu ya uovu wake.

19. Na mtu mwovu akiacha uovu wake, akaanza kutenda mambo ya haki na mema ataishi kwa sababu ya matendo yake mema.

Kusoma sura kamili Ezekieli 33