Agano la Kale

Agano Jipya

Ezekieli 20:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Mwaka wa saba tangu kuhamishwa kwetu, siku ya kumi ya mwezi wa tano, baadhi ya wazee wa Israeli walikuja kumwuliza Mwenyezi-Mungu shauri, wakaketi mbele yangu.

2. Basi, neno la Mwenyezi-Mungu likanijia:

3. “Wewe mtu, sema na hao wazee wa Israeli. Waambie kuwa mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Je, mmekuja kuniuliza shauri? Hakika, kama niishivyo mimi Bwana Mwenyezi-Mungu, nasema kuwa sitakubali kuulizwa kitu na nyinyi.

4. “Wewe mtu, je, uko tayari kuwahukumu watu hawa? Basi, wahukumu. Wajulishe waliyofanya wazee wao.

5. Waambie kwamba mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Siku ile nilipowachagua Waisraeli niliwaapia wazawa wa Yakobo. Nilijidhihirisha kwao nchini Misri, nikawaapia nikisema: Mimi ni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.

6. Siku hiyo niliwaapia kwamba nitawatoa nchini Misri na kuwaongoza mpaka kwenye nchi niliyowachagulia, nchi inayotiririka maziwa na asali na nchi nzuri kuliko nchi zote.

7. Niliwaambia: ‘Tupilieni mbali machukizo yote mnayoyapenda; msijitie unajisi kwa sanamu za miungu ya Misri, kwa maana mimi ni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.’

8. Lakini waliniasi, hawakutaka kunisikiliza. Hakuna hata mmoja wao aliyetupilia mbali machukizo yale waliyoyapenda, wala hawakuachana na sanamu za miungu ya Misri. Basi, nikafikiri kwamba nitawamwagia ghadhabu yangu na kuitimiza hasira yangu juu yao wakiwa kulekule nchini Misri.

9. Lakini nilijizuia kufanya hivyo kwa heshima ya jina langu ili lisidharauliwe kati ya watu wa mataifa wanaoishi nao, hao walioona nikijijulisha kwa Waisraeli wakati wa kuwatoa katika nchi ya Misri.

10. “Basi, mimi niliwatoa nchini Misri, nikawapeleka jangwani.

11. Niliwapa kanuni zangu na kuwafundisha amri zangu ambazo mtu akizifuata huishi.

12. Niliwapa pia Sabato zangu ziwe ishara kati yangu na wao, wapate kujua kuwa mimi ni Mwenyezi-Mungu ninayewatakasa.

Kusoma sura kamili Ezekieli 20