Agano la Kale

Agano Jipya

Danieli 6:9-19 Biblia Habari Njema (BHN)

9. Hivyo, mfalme Dario akaitia sahihi hati ya sheria hiyo.

10. Danieli alipojua kuwa ile hati imetiwa sahihi, alirudi nyumbani kwake ghorofani katika chumba chake kilichokuwa na madirisha yaliyofunguka kuelekea Yerusalemu. Humo, Danieli, kama ilivyokuwa kawaida yake, alipiga magoti mara tatu kila siku akamwomba na kumshukuru Mungu wake.

11. Watu wale waliofanya mpango dhidi ya Danieli waliingia ndani, wakamkuta Danieli akiomba dua na kumsihi Mungu wake.

12. Basi, walikwenda kwa mfalme na kumshtaki Danieli kwa kutumia ile sheria, wakisema, “Mfalme Dario, je, hukutia sahihi hati ya sheria kuwa kwa muda wa siku thelathini hakuna mtu yeyote atakayeruhusiwa kuomba kitu chochote, kwa mungu yeyote, au kwa mtu yeyote isipokuwa kutoka kwako wewe, ee mfalme, na kwamba yeyote atakayevunja sheria hii atatumbukizwa katika pango la simba?” Mfalme akaitikia, “Hivyo ndivyo ilivyo, kulingana na sheria ya Wamedi na Wapersi ambayo haiwezi kubatilishwa.”

13. Wakamwambia mfalme, “Yule Danieli aliye mmoja wa mateka kutoka nchi ya Yuda hakuheshimu wewe mfalme wala haitii amri uliyotia sahihi. Yeye anasali mara tatu kila siku.”

14. Mfalme aliposikia maneno hayo, alisikitika sana. Akajitahidi sana kupata njia ya kumwokoa Danieli. Aliendelea kujaribu mpaka jua likatua.

15. Wale watu wakamwendea mfalme Dario kwa pamoja na kumwambia, “Ee mfalme, ujue kuwa hakuna sheria wala amri yoyote ya Wamedi na Wapersi inayoweza kubatilishwa baada ya kuwekwa na mfalme.”

16. Ndipo mfalme Dario akatoa amri, naye Danieli akaletwa na kutupwa katika pango la simba. Mfalme akamwambia Danieli, “Mungu wako ambaye unamtumikia daima, na akuokoe.”

17. Jiwe likaletwa na kuwekwa mlangoni mwa lile pango. Mfalme akalipiga mhuri wake binafsi na ule wa wakuu wake, ili uamuzi kuhusu Danieli usibatilishwe.

18. Kisha mfalme akarudi katika ikuluni yake ambamo alikesha akifunga; hakufanya tafrija ya aina yoyote, na usingizi ukampaa.

19. Alfajiri na mapema, mfalme Dario aliamka, akaenda kwa haraka kwenye pango la simba.

Kusoma sura kamili Danieli 6