Agano la Kale

Agano Jipya

2 Wafalme 9:25-36 Biblia Habari Njema (BHN)

25. Yehu akamwambia msaidizi wake Bidkari, “Chukua hiyo maiti yake uitupe katika shamba hilo la Nabothi Myezreeli. Kwa maana, kumbuka wewe na mimi tulipokuwa tumepanda farasi wetu nyuma ya baba yake Ahabu, jinsi Mwenyezi-Mungu alivyonena maneno haya dhidi yake.

26. Mwenyezi-Mungu alisema, ‘Kwa ile damu ya Nabothi na kwa damu ya wanawe niliyoona jana naapa kwamba nitakulipiza kisasi katika shamba hilo.’ Kwa hiyo, chukua maiti ya Yoramu uitupe katika shamba la Nabothi kama alivyosema Mwenyezi-Mungu.”

27. Ahazia mfalme wa Yuda alipoona yaliyotukia alikimbia akielekea Nyumba ya Bustani, huku akifuatwa na Yehu. Yehu akawaamuru watu wake, “Muueni naye pia!” Nao wakampiga mshale akiwa garini kwenye njia ya kupanda Guri karibu na mji wa Ibleamu. Halafu alikimbilia Megido na kufia huko.

28. Maofisa wake wakaichukua maiti yake ndani ya gari lake na kuipeleka Yerusalemu; na huko akazikwa katika makaburi ya kifalme katika mji wa Daudi.

29. Ahazia alianza kutawala juu ya Yuda katika mwaka wa kumi na moja wa enzi ya Yoramu mwana wa Ahabu.

30. Yehu alipofika Yezreeli, Yezebeli alikuwa amekwisha pata habari za mambo yaliyotokea. Alijipaka rangi machoni na kupanga nywele zake, ndipo akaenda dirishani na kuangalia chini.

31. Yehu alipokuwa akiingia langoni Yezebeli alisema, “Unakuja kwa amani, ewe Zimri! Wewe unayewaua mabwana zako?”

32. Yehu akaangalia juu na kusema “Ni nani aliye upande wangu?” Maofisa wawili au watatu wakatokeza vichwa vyao kumwangalia kutoka dirishani,

33. naye Yehu akawaambia, “Mtupe chini!” Wakamtupa chini na damu yake ikatapakaa juu ya ukuta na kwenye farasi. Yehu akapitisha farasi na gari lake juu ya maiti yake

34. na kuingia katika jumba la kifalme, na huko akala na kunywa. Halafu akaamuru: “Mzikeni mwanamke huyo aliyelaaniwa; kwa kuwa ni binti mfalme.”

35. Ndipo walipokwenda kumzika; lakini hawakuona chochote isipokuwa fuvu la kichwa, mifupa ya mikono na miguu.

36. Kisha walirudi na kumpasha Yehu habari hizi, naye akasema, “Hivi ndivyo Mwenyezi-Mungu alivyotabiri kupitia kwa mtumishi wake Elia Mtishbi akisema, ‘Mbwa wataula mwili wa Yezebeli katika nchi ya Yezreeli.

Kusoma sura kamili 2 Wafalme 9