Agano la Kale

Agano Jipya

2 Wafalme 25:22-30 Biblia Habari Njema (BHN)

22. Mfalme Nebukadneza wa Babuloni alimteua Gedalia mwana wa Ahikamu, mjukuu wa Shafani, kuwa mtawala wa watu wote wa Yuda ambao hawakupelekwa Babuloni.

23. Kisha makapteni wote wa majeshi pamoja na watu wao waliposikia kuwa mfalme wa Babuloni alimteua Gedalia kuwa mtawala, walimwendea Gedalia huko Mizpa. Watu hao walikuwa Ishmaeli mwana wa Nethania, Yohanani mwana wa Karea, Seraya mwana wa Tanhumethi Mnetofathi, na Yezania mwana wa Mmaaka.

24. Naye Gedalia aliapa mbele yao na watu wao, akasema, “Msiogope kwa sababu ya maofisa wa Wakaldayo. Kaeni nchini mumtumikie mfalme wa Babuloni na mambo yote yatawaendea vema.”

25. Mnamo mwezi wa saba, Ishmaeli mwana wa Nethania, mjukuu wa Elishama aliyekuwa wa ukoo wa kifalme, alifika kwa Gedalia akiandamana na watu kumi, akamshambulia Gedalia, akamuua. Vilevile, aliwaua Wayahudi na Wakaldayo waliokuwa naye.

26. Halafu, Waisraeli wote, wadogo kwa wakubwa pamoja na maofisa wa majeshi, waliondoka, wakaenda Misri, kwa sababu waliwaogopa Wakaldayo.

27. Mnamo mwaka wa thelathini na mbili, Evil-merodaki mfalme wa Babuloni, alipoanza kutawala, mwaka huohuo alimsamehe Yehoyakini mfalme wa Yuda, akamtoa gerezani. Hiyo ilikuwa siku ya ishirini na saba ya mwezi wa kumi na mbili, mwaka wa thelathini na saba tangu Yehoyakini alipochukuliwa mateka.

28. Aliongea naye vizuri na kumpa nafasi ya heshima kuliko wafalme wengine waliokuwa pamoja naye huko Babuloni.

29. Basi, Yehoyakini alibadili mavazi yake ya kifungoni. Kila siku alikuwa anapata daima chakula chake kwa mfalme.

30. Alipatiwa na mfalme mahitaji yake siku kwa siku, maisha yake yote.

Kusoma sura kamili 2 Wafalme 25