Agano la Kale

Agano Jipya

2 Wafalme 22:4-17 Biblia Habari Njema (BHN)

4. “Nenda kwa kuhani mkuu Hilkia umwambie ahesabu zile fedha zilizoletwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu ambazo mabawabu walizikusanya kutoka kwa watu.

5. Kiasi cha fedha hizo zipewe wasimamizi wa marekebisho ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu kulipa mishahara ya mafundi wanaofanya marekebisho,

6. yaani maseremala, wajenzi na waashi. Kiasi kingine kitumike kununua mbao na mawe yaliyochongwa kwa ajili ya kurekebisha nyumba.

7. Watu wanaosimamia ujenzi wasidaiwe kutoa hesabu ya matumizi ya fedha watakazokabidhiwa, kwa sababu wanazitumia kwa uaminifu.”

8. Kisha kuhani mkuu Hilkia alimwambia katibu Shafani, “Nimekipata Kitabu cha Sheria katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu.” Halafu Hilkia akampatia Shafani kitabu, naye akakisoma.

9. Katibu Shafani, alimwendea mfalme na kutoa habari, akisema, “Watumishi wako wametoa fedha zilizopatikana katika nyumba halafu wamezikabidhi kwa mafundi wanaosimamia marekebisho ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu.”

10. Kisha katibu Shafani, akamwambia mfalme, “Kuhani Hilkia amenipa kitabu.” Naye Shafani akakisoma mbele ya mfalme.

11. Mfalme aliposikia maneno ya Kitabu cha Sheria, alirarua mavazi yake.

12. Mara aliamuru kuhani Hilkia, Ahikamu mwana wa Shafani na Akbori mwana wa Mikaya pamoja na katibu Shafani na Asaya mtumishi wa mfalme, akisema,

13. “Nendeni mkatafute shauri kutoka kwa Mwenyezi-Mungu kwa niaba yangu na watu wa Yuda wote kuhusu maneno ya kitabu hiki kilichopatikana kwa sababu ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu imewaka juu yetu, maana babu zetu hawakutii maneno ya kitabu hiki, na kutimiza yote yaliyoandikwa kutuhusu.”

14. Kwa hiyo kuhani Hilkia, Ahikamu, Akbori, Shafani na Asaya, wote walikwenda kwa mama mmoja nabii jina lake Hulda aliyekuwa mke wa Shalumu, mwana wa Tikva, mwana wa Harhasi, mtunza mavazi ya hekalu. Wakati huo Hulda alikuwa anaishi katika mtaa wa pili wa Yerusalemu, nao wakazungumza naye.

15. Basi akawaambia, “Hivi ndivyo anavyosema Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli: ‘Mwambie huyo aliyewatuma kwangu,

16. Mwenyezi-Mungu anasema hivi: Nitaleta uovu juu ya mahali hapa na juu ya wakazi wake kama ilivyo katika kitabu kilichosomwa na mfalme wa Yuda.

17. Kwa sababu wameniacha na kufukizia ubani miungu mingine na hivyo kunikasirisha kwa kazi zote za mikono yao, ghadhabu yangu dhidi ya Yerusalemu itawaka na haitaweza kutulizwa.

Kusoma sura kamili 2 Wafalme 22