Agano la Kale

Agano Jipya

2 Samueli 3:18-29 Biblia Habari Njema (BHN)

18. Sasa, lileteni jambo hilo hadharani kwa sababu Mwenyezi-Mungu alimwahidi hivi Daudi, ‘Kwa mkono wako wewe Daudi mtumishi wangu, nitawaokoa watu wangu wa Israeli kutoka kwa Wafilisti na kutoka kwa adui zao wengine.’”

19. Abneri pia akazungumza na Wabenyamini, kisha akaenda mpaka Hebroni kumwambia Daudi kuhusu yale ambayo watu wote wa Israeli na kabila lote la Benyamini walipatana kutenda.

20. Abneri alipomwendea Daudi, alikuwa na watu ishirini, Daudi aliwafanyia karamu.

21. Abneri akamwambia Daudi, “Mimi sasa nitakwenda na kukuletea watu wote wa Israeli, wewe bwana wangu mfalme. Watakuja na kufanya agano nawe, ili uwe mfalme wao, nawe utawatawala wote kama upendavyo.” Daudi akamuaga Abneri aende zake, naye akaondoka kwa amani.

22. Baadaye, Yoabu na baadhi ya watu wa Daudi walirudi kutoka mashambulio, wakaleta nyara nyingi. Lakini Abneri hakuwa pamoja na Daudi huko Hebroni kwani Daudi alikuwa amemuaga aende zake, naye akaondoka kwa amani.

23. Yoabu aliporudi akiwa na jeshi lake lote alilokuwa nalo, aliambiwa kwamba Abneri mwana wa Neri, alikuwa amekuja kumwona mfalme Daudi, naye amemuaga aende zake, naye ameondoka kwa amani.

24. Yoabu alimwendea mfalme na kumwambia, “Sasa umefanya nini? Tazama Abneri alikuja kwako, kwa nini umemwacha aende?

25. Je, unajua kuwa Abneri mwana wa Neri alikuja kukudanganya? Alikuja ili ajue mienendo yako na yale unayoyafanya.”

26. Yoabu alipotoka kuzungumza na Daudi, alituma wajumbe wakamlete Abneri, nao wakamkuta kwenye kisima cha Sira na kumrudisha, lakini Daudi hakujua jambo hilo.

27. Abneri aliporudi Hebroni, Yoabu alimchukua kando kwenye lango kana kwamba anataka kuzungumza naye kwa faragha. Hapo Yoabu akamkata Abneri tumboni kwa sababu Abneri alikuwa amemuua Asaheli ndugu yake, na Abneri akafa.

28. Baadaye Daudi aliposikia habari hizo alisema, “Mimi na ufalme wangu hatuna hatia mbele ya Mwenyezi-Mungu kuhusu damu ya Abneri mwana wa Neri.

29. Lawama ya mauaji hayo yawe juu ya kichwa cha Yoabu na jamaa yote ya baba yake! Jamaa ya Yoabu daima isikose mtu mwenye ugonjwa wa kisonono, au ugonjwa wa ukoma, au anayetembea kwa magogo au kuuawa kwa upanga, au mwenye kukosa chakula!”

Kusoma sura kamili 2 Samueli 3