Agano la Kale

Agano Jipya

2 Samueli 3:10-22 Biblia Habari Njema (BHN)

10. Mwenyezi-Mungu alimwapia Daudi kuwa atauhamisha ufalme kutoka jamaa ya Shauli na kumpa yeye. Naye atatawala Israeli na Yuda kutoka Dani hadi Beer-sheba.”

11. Ishboshethi hakuweza kusema neno, kwa kuwa alikuwa anamwogopa Abneri.

12. Basi, Abneri akatuma wajumbe kwa Daudi, huko Hebroni wakamwambie, “Je, nchi hii ni mali ya nani? Fanya agano na mimi, nami nitakusaidia kuifanya Israeli yote iwe chini yako.”

13. Daudi akamjibu, “Vema, nitafanya agano nawe. Lakini ninakutaka jambo moja kwamba kabla hujaniona sharti kwanza uniletee Mikali binti wa Shauli. Hapo utaniona.”

14. Daudi pia alituma wajumbe kwa Ishboshethi mwana wa Shauli akisema, “Nirudishie mke wangu Mikali ambaye nilimwoa kwa magovi 100 ya Wafilisti.”

15. Basi, Ishboshethi alituma watu wakamchukue Mikali kutoka kwa mumewe, Paltieli mwana wa Laishi.

16. Lakini Paltieli akaenda pamoja na mkewe huku analia njia nzima mpaka huko Bahurimu. Abneri akamwambia Paltieli, “Rudi nyumbani.” Naye akarudi.

17. Abneri alifanya mashauri na wazee wa Israeli, akawaambia, “Kwa muda fulani uliopita mmekuwa mkitaka Daudi awe mfalme wenu.

18. Sasa, lileteni jambo hilo hadharani kwa sababu Mwenyezi-Mungu alimwahidi hivi Daudi, ‘Kwa mkono wako wewe Daudi mtumishi wangu, nitawaokoa watu wangu wa Israeli kutoka kwa Wafilisti na kutoka kwa adui zao wengine.’”

19. Abneri pia akazungumza na Wabenyamini, kisha akaenda mpaka Hebroni kumwambia Daudi kuhusu yale ambayo watu wote wa Israeli na kabila lote la Benyamini walipatana kutenda.

20. Abneri alipomwendea Daudi, alikuwa na watu ishirini, Daudi aliwafanyia karamu.

21. Abneri akamwambia Daudi, “Mimi sasa nitakwenda na kukuletea watu wote wa Israeli, wewe bwana wangu mfalme. Watakuja na kufanya agano nawe, ili uwe mfalme wao, nawe utawatawala wote kama upendavyo.” Daudi akamuaga Abneri aende zake, naye akaondoka kwa amani.

22. Baadaye, Yoabu na baadhi ya watu wa Daudi walirudi kutoka mashambulio, wakaleta nyara nyingi. Lakini Abneri hakuwa pamoja na Daudi huko Hebroni kwani Daudi alikuwa amemuaga aende zake, naye akaondoka kwa amani.

Kusoma sura kamili 2 Samueli 3