Agano la Kale

Agano Jipya

2 Samueli 19:18-34 Biblia Habari Njema (BHN)

18. Basi, wakavuka kwenye kivuko ili kuisindikiza jamaa ya mfalme na kumfanyia mfalme yote aliyoyapenda. Shimei mwana wa Gera akaja, akajitupa mbele ya mfalme, akasujudu, wakati mfalme alipokuwa karibu kuvuka mto Yordani.

19. Shimei akamwambia mfalme, “Nakuomba, bwana wangu mfalme, usinihesabu kuwa na hatia wala kukumbuka kosa nililofanya siku ile ulipokuwa ukiondoka mjini Yerusalemu. Nakuomba usiyaweke hayo maanani.

20. Maana, mimi mtumishi wako ninajua kwamba nilitenda dhambi. Hii ndiyo sababu nimekuja leo, nikiwa wa kwanza katika kabila la Yosefu, kuja kukulaki wewe bwana wangu, mfalme.”

21. Ndipo Abishai mwana wa Seruya akasema, “Je, si lazima Shimei auawe maana alimlaani mtu ambaye Mwenyezi-Mungu amemteua kwa kumpaka mafuta?”

22. Lakini Daudi akasema, “Wana wa Seruya, sina lolote nanyi; kwa nini mjifanye kama maadui zangu leo? Je, auawe mtu yeyote katika Israeli siku ya leo? Je, sijui kuwa mimi ni mfalme wa Israeli siku ya leo?”

23. Kisha, mfalme akamwambia Shimei, “Wewe hutauawa.” Mfalme akamwapia Shimei.

24. Mefiboshethi mjukuu wa Shauli, alikwenda pia kumlaki mfalme Daudi. Tangu siku ile mfalme alipoondoka Yerusalemu mpaka aliporudi salama, Mefiboshethi alikuwa hajapata kuosha miguu yake, kukata ndevu zake na hakujali kufua nguo zake.

25. Basi, ikawa alipofika Yerusalemu kumlaki mfalme, Daudi alimwuliza, “Je, Mefiboshethi, kwa nini hukuandamana pamoja nami?”

26. Mefiboshethi akasema, “Ee bwana wangu mfalme, mtumishi wangu alinidanganya. Maana, mimi mtumishi wako, nilimwambia, ‘Nitandikie punda nipate kumpanda kwenda pamoja na mfalme,’ maana mimi mtumishi wako ni kilema.

27. Sasa, amenisingizia kwako, ee bwana wangu mfalme. Lakini wewe, bwana wangu mfalme, uko kama malaika wa Mungu. Fanya lolote unaloona ni jema kwako.

28. Maana, jamaa yote ya babu yangu walikuwa watu ambao wamestahili kuuawa mbele yako, bwana wangu mfalme. Lakini uliniweka mimi mtumishi wako miongoni mwa wale wanaokula mezani pako. Je, nina haki yoyote zaidi hata nikulilie mfalme?”

29. Mfalme akamwambia, “Usiniambie zaidi juu ya mambo yako ya binafsi. Mimi nimekwisha amua kuwa wewe pamoja na Siba mtagawana nchi ya Shauli.”

30. Lakini Mefiboshethi akamwambia mfalme, “Mruhusu Siba aichukue nchi yote peke yake. Mimi nimetosheka kwamba wewe bwana wangu mfalme umerudi nyumbani salama.”

31. Barzilai Mgileadi alikuwa amefika kutoka Rogelimu. Alikuwa amekwenda pamoja na mfalme kwenye mto Yordani ili kumsindikiza hadi ngambo ya mto.

32. Barzilai alikuwa mzee sana, mwenye umri wa miaka themanini. Naye Barzilai alikuwa amemtunza mfalme alipokaa huko Mahanaimu, kwa kuwa alikuwa tajiri sana.

33. Basi, mfalme Daudi akamwambia Barzilai, “Twende wote huko Yerusalemu nami nitakutunza.”

34. Lakini Barzilai akamwambia mfalme, “Je, nina miaka mingi ya kuishi ndipo niende nawe mfalme mpaka Yerusalemu?

Kusoma sura kamili 2 Samueli 19