Agano la Kale

Agano Jipya

2 Samueli 15:12-25 Biblia Habari Njema (BHN)

12. Wakati Absalomu alipokuwa akitoa tambiko, alituma ujumbe mjini Gilo kumwita Ahithofeli, Mgilo, aliyekuwa mshauri wa mfalme Daudi. Uasi wa Absalomu ukazidi kupata nguvu na watu walioandamana naye wakazidi kuongezeka.

13. Mjumbe fulani alipomwendea Daudi na kumwambia, “Watu wa Israeli wamevutwa na Absalomu!”

14. Basi, Daudi akawaambia watumishi wake waliokuwa naye mjini Yerusalemu, “Inukeni tukimbie, la sivyo, hatutaweza kumwepa Absalomu. Tufanye haraka kuondoka asije akatuletea maafa na kuuangamiza mji kwa mapanga.”

15. Lakini watumishi wake wakamwambia, “Sisi watumishi wako, bwana wetu mfalme, tuko tayari kufanya lolote unaloamua.”

16. Basi, mfalme akaondoka pamoja na jamaa yake, lakini akawaacha masuria wake kumi wakishughulika na kazi za nyumbani.

17. Mfalme akaondoka pamoja na watu wake wote. Lakini akatua kidogo walipofikia nyumba ya mwisho mjini.

18. Watumishi wote wa mfalme, Wakerethi wote, Wapelethi wote, pamoja na Wagiti 600 waliomfuata mfalme Daudi kutoka mji wa Gathi, waliondoka pamoja naye wakimtangulia.

19. Kisha, mfalme Daudi alipomwona Itai, Mgiti, alimwambia, “Kwa nini hata wewe umeondoka pamoja nasi? Rudi ukakae na huyo mfalme kijana. Maana wewe ni mgeni huku, tena ni mkimbizi kutoka nyumbani kwenu.

20. Wewe ulikuja huku juzijuzi tu. Je, nikufanye mtu wa kutangatanga pamoja nasi, nikijua kuwa sijui hata kule ninakoenda? Rudi nyumbani pamoja na ndugu zako. Naye Mwenyezi-Mungu akuoneshe fadhili zake na uaminifu.”

21. Lakini Itai akamjibu mfalme, “Kama Mwenyezi-Mungu aishivyo na wewe bwana wangu mfalme uishivyo, popote utakapokuwa, ikiwa ni kwa kufa au ni kwa kuishi, nami mtumishi wako nitakuwapo.”

22. Basi, Daudi akamwambia Itai, “Nenda basi, endelea mbele.” Hivyo, Itai, Mgiti, akapita yeye mwenyewe pamoja na watoto wake.

23. Daudi alipokuwa akipita pamoja na watu wake, watu wote nchini kote walilia kwa sauti. Mfalme Daudi akavuka kijito cha Kidroni pamoja na watu wote, wakapita kuelekea jangwani.

24. Kuhani Abiathari akatoka, hata na kuhani Sadoki akatoka pamoja na Walawi wote huku wamelibeba sanduku la agano la Mungu. Wakaliweka chini lile sanduku la Mungu, mpaka watu wote walipopita kutoka mjini Yerusalemu.

25. Kisha mfalme akamwambia Sadoki, “Lirudishe sanduku la agano la Mungu mjini. Kama ninakubalika mbele ya Mwenyezi-Mungu, bila shaka atanirudisha na kunijalia kuliona tena sanduku lake na kuyaona maskani yake.

Kusoma sura kamili 2 Samueli 15