Agano la Kale

Agano Jipya

2 Samueli 15:11-21 Biblia Habari Njema (BHN)

11. Absalomu alipokwenda huko Hebroni, alikwenda na watu 200 aliowaalika kutoka Yerusalemu, nao walikwenda huko kwa nia njema, wala hawakujua chochote kuhusu mpango wa Absalomu.

12. Wakati Absalomu alipokuwa akitoa tambiko, alituma ujumbe mjini Gilo kumwita Ahithofeli, Mgilo, aliyekuwa mshauri wa mfalme Daudi. Uasi wa Absalomu ukazidi kupata nguvu na watu walioandamana naye wakazidi kuongezeka.

13. Mjumbe fulani alipomwendea Daudi na kumwambia, “Watu wa Israeli wamevutwa na Absalomu!”

14. Basi, Daudi akawaambia watumishi wake waliokuwa naye mjini Yerusalemu, “Inukeni tukimbie, la sivyo, hatutaweza kumwepa Absalomu. Tufanye haraka kuondoka asije akatuletea maafa na kuuangamiza mji kwa mapanga.”

15. Lakini watumishi wake wakamwambia, “Sisi watumishi wako, bwana wetu mfalme, tuko tayari kufanya lolote unaloamua.”

16. Basi, mfalme akaondoka pamoja na jamaa yake, lakini akawaacha masuria wake kumi wakishughulika na kazi za nyumbani.

17. Mfalme akaondoka pamoja na watu wake wote. Lakini akatua kidogo walipofikia nyumba ya mwisho mjini.

18. Watumishi wote wa mfalme, Wakerethi wote, Wapelethi wote, pamoja na Wagiti 600 waliomfuata mfalme Daudi kutoka mji wa Gathi, waliondoka pamoja naye wakimtangulia.

19. Kisha, mfalme Daudi alipomwona Itai, Mgiti, alimwambia, “Kwa nini hata wewe umeondoka pamoja nasi? Rudi ukakae na huyo mfalme kijana. Maana wewe ni mgeni huku, tena ni mkimbizi kutoka nyumbani kwenu.

20. Wewe ulikuja huku juzijuzi tu. Je, nikufanye mtu wa kutangatanga pamoja nasi, nikijua kuwa sijui hata kule ninakoenda? Rudi nyumbani pamoja na ndugu zako. Naye Mwenyezi-Mungu akuoneshe fadhili zake na uaminifu.”

21. Lakini Itai akamjibu mfalme, “Kama Mwenyezi-Mungu aishivyo na wewe bwana wangu mfalme uishivyo, popote utakapokuwa, ikiwa ni kwa kufa au ni kwa kuishi, nami mtumishi wako nitakuwapo.”

Kusoma sura kamili 2 Samueli 15