Agano la Kale

Agano Jipya

2 Mambo Ya Nyakati 29:21-28 Biblia Habari Njema (BHN)

21. Wakaleta mafahali saba, kondoo madume saba, wanakondoo saba na mbuzi madume saba, wawe sadaka ya kuondoa dhambi, kwa ajili ya jamaa ya kifalme, patakatifu na watu wa Yuda. Hapo, mfalme aliwaambia makuhani waliokuwa wazawa wa Aroni wawateketeze juu ya madhabahu ya Mwenyezi-Mungu.

22. Makuhani walichinja mafahali kwanza, kisha kondoo madume, halafu wanakondoo na kila mara walichukua damu ya wanyama hao na kunyunyiza juu ya madhabahu.

23. Hatimaye, waliwaleta wale mbuzi madume wa sadaka ya kuondoa dhambi karibu na mfalme na watu wote waliokuwamo, nao wakaweka mikono yao juu ya hao mbuzi madume.

24. Basi, wale makuhani wakawachinja, na kunyunyiza damu yao juu ya madhabahu ili iwe tambiko ya upatanisho kwa Waisraeli wote, kwa maana mfalme Hezekia alikuwa ameagiza itolewe sadaka ya kuteketeza na sadaka ya kuondoa dhambi kwa ajili ya Israeli yote.

25. Mfalme Hezekia aliyafuata maagizo ambayo Mwenyezi-Mungu alikuwa amempa mfalme Daudi kwa njia ya Gadi mwonaji wa mfalme na nabii Nathani. Hivyo basi, akaweka Walawi katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, baadhi yao wakiwa na matoazi, wengine vinanda na wengine vinubi. Hiyo ilikuwa amri ya Mwenyezi-Mungu kwa njia ya manabii wake.

26. Walawi walisimama na vyombo vya muziki vya Daudi, pia makuhani walisimama wakiwa na tarumbeta zao.

27. Basi, Hezekia akaamuru sadaka ya kuteketeza itolewe juu ya madhabahu. Mara tu tambiko hiyo ilipoanza kutolewa, watu walianza kumsifu Mwenyezi-Mungu kwa nyimbo zilizoandamana na mlio wa tarumbeta na vyombo vya muziki vya Daudi mfalme wa Israeli.

28. Watu wote waliokuwamo walishiriki katika ibada. Waimbaji waliendelea kuimba, na tarumbeta zikaendelea kupigwa hadi shughuli za utoaji wa sadaka hiyo ya kuteketeza ilipokamilika.

Kusoma sura kamili 2 Mambo Ya Nyakati 29