Agano la Kale

Agano Jipya

2 Mambo Ya Nyakati 29:19-36 Biblia Habari Njema (BHN)

19. Tena, vyombo vyote ambavyo mfalme Ahazi alivyoviondoa wakati wa utawala wake, hapo alipoasi, tumevirudisha na kuviweka wakfu. Vyote vipo mbele ya madhabahu ya Mwenyezi-Mungu.”

20. Mapema kesho yake, mfalme Hezekia aliwakusanya wakuu wa mji, akaenda nao katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu.

21. Wakaleta mafahali saba, kondoo madume saba, wanakondoo saba na mbuzi madume saba, wawe sadaka ya kuondoa dhambi, kwa ajili ya jamaa ya kifalme, patakatifu na watu wa Yuda. Hapo, mfalme aliwaambia makuhani waliokuwa wazawa wa Aroni wawateketeze juu ya madhabahu ya Mwenyezi-Mungu.

22. Makuhani walichinja mafahali kwanza, kisha kondoo madume, halafu wanakondoo na kila mara walichukua damu ya wanyama hao na kunyunyiza juu ya madhabahu.

23. Hatimaye, waliwaleta wale mbuzi madume wa sadaka ya kuondoa dhambi karibu na mfalme na watu wote waliokuwamo, nao wakaweka mikono yao juu ya hao mbuzi madume.

24. Basi, wale makuhani wakawachinja, na kunyunyiza damu yao juu ya madhabahu ili iwe tambiko ya upatanisho kwa Waisraeli wote, kwa maana mfalme Hezekia alikuwa ameagiza itolewe sadaka ya kuteketeza na sadaka ya kuondoa dhambi kwa ajili ya Israeli yote.

25. Mfalme Hezekia aliyafuata maagizo ambayo Mwenyezi-Mungu alikuwa amempa mfalme Daudi kwa njia ya Gadi mwonaji wa mfalme na nabii Nathani. Hivyo basi, akaweka Walawi katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, baadhi yao wakiwa na matoazi, wengine vinanda na wengine vinubi. Hiyo ilikuwa amri ya Mwenyezi-Mungu kwa njia ya manabii wake.

26. Walawi walisimama na vyombo vya muziki vya Daudi, pia makuhani walisimama wakiwa na tarumbeta zao.

27. Basi, Hezekia akaamuru sadaka ya kuteketeza itolewe juu ya madhabahu. Mara tu tambiko hiyo ilipoanza kutolewa, watu walianza kumsifu Mwenyezi-Mungu kwa nyimbo zilizoandamana na mlio wa tarumbeta na vyombo vya muziki vya Daudi mfalme wa Israeli.

28. Watu wote waliokuwamo walishiriki katika ibada. Waimbaji waliendelea kuimba, na tarumbeta zikaendelea kupigwa hadi shughuli za utoaji wa sadaka hiyo ya kuteketeza ilipokamilika.

29. Hatimaye, mfalme Hezekia pamoja na watu wote waliokuwamo waliinama, wakamwabudu Mwenyezi-Mungu.

30. Kisha mfalme Hezekia na viongozi wakawaambia Walawi wamsifu Mwenyezi-Mungu kwa nyimbo alizotunga mfalme Daudi na mwonaji Asafu. Basi, watu wote wakamtukuza Mungu kwa furaha, na kumsujudia.

31. Ndipo Hezekia akawaambia watu, “Maadamu sasa mmekwisha jitakasa, karibieni, leteni sadaka na matoleo ya shukrani katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu.” Basi, watu wakaleta sadaka zao na matoleo yao ya shukrani, na tambiko za kuteketeza.

32. Sadaka za kuteketeza walizoleta jumla zilikuwa mafahali 70, kondoo madume 100 na wanakondoo 200. Zote hizo zilikuwa sadaka za kuteketeza kwa Mwenyezi-Mungu.

33. Matoleo matakatifu yalikuwa mafahali 600 na kondoo 3,000.

34. Kwa vile ambavyo idadi ya makuhani ilikuwa ndogo, hawakuweza kuwachuna wanyama hao wote. Kwa hiyo, ndugu zao Walawi waliwasaidia hadi walipokamilisha kazi hiyo. Wakati huo, makuhani wengine zaidi walikuwa wamekwisha jitakasa. (Walawi walijiweka katika hali ya usafi zaidi kuliko makuhani.)

35. Mbali na wingi wa sadaka za kuteketeza, kulikuwako pia mafuta ya sadaka ya amani, hata kulikuwapo sadaka ya kinywaji kwa sadaka za kuteketeza. Hivyo basi, huduma za ibada zikaanzishwa tena hekaluni.

36. Mfalme Hezekia na watu wote wakajawa na furaha tele kwa sababu ya yote Mungu aliyowatendea watu; maana tukio hili lilitokea ghafla.

Kusoma sura kamili 2 Mambo Ya Nyakati 29