Agano la Kale

Agano Jipya

2 Mambo Ya Nyakati 11:1-18 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Rehoboamu alipofika Yerusalemu, alikusanya askari stadi180,000 wa makabila ya Yuda na Benyamini, apate kupigana na Israeli, ili ajirudishie huo ufalme.

2. Lakini ujumbe wa Mungu ulimjia Shemaya mtu wa Mungu, kusema:

3. “Mwambie Rehoboamu mwana wa Solomoni, mfalme wa Yuda na Waisraeli wote katika Yuda na Benyamini ya kwamba

4. mimi Bwana nasema, ‘Msiende wala msipigane na ndugu zenu. Rudini kila mtu nyumbani kwake, maana hayo yaliyotokea ni kama nilivyopanga.’” Basi wakatii ujumbe wa Mwenyezi-Mungu, wakarudi nyumbani, wala hawakwenda kupigana na Yeroboamu.

5. Rehoboamu alikaa Yerusalemu na akajenga ngome na kuiimarisha miji ifuatayo iliyokuwa nchini Yuda:

6. Bethlehemu, Etamu, Tekoa,

7. Beth-suri, Soko, Adulamu,

8. Gathi, Maresha, Zifu,

9. Adoraimu, Lakishi, Azeka,

10. Sora, Ayaloni na Hebroni. Miji hiyo yenye ngome imo Yuda na Benyamini.

11. Aliziimarisha ngome hizo na humo ndani akaweka makamanda na maghala ya vyakula, mafuta na divai.

12. Ndani ya kila mji, aliweka ngao na mikuki, na kuifanya miji hiyo kuwa imara sana. Yuda na Benyamini zikawa chini ya mamlaka yake.

13. Makuhani na Walawi wote waliokuwa wanaishi kote nchini Israeli, walimwendea kutoka maeneo yao.

14. Walawi waliyaacha malisho yao, na maeneo yao mengine kwa sababu Yeroboamu na wanawe waliwakataza kumtumikia Mwenyezi-Mungu kama makuhani wa Mwenyezi-Mungu.

15. Yeroboamu alijichagulia makuhani wake mwenyewe wa kuhudumu mahali pa juu pa kuabudia miungu na yale majini na sanamu za ndama alizojitengenezea.

16. Watu wote ambao walikuwa wamenuia kwa moyo wa dhati kumwabudu Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kutoka katika makabila yote ya Israeli, waliandamana na Walawi hadi Yerusalemu ili wapate kumtolea tambiko Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zao.

17. Hivyo, waliuimarisha ufalme wa Yuda, na kwa muda wa miaka mitatu, wakauunga mkono utawala wa Rehoboamu mwanawe Solomoni, nao ukawa imara na wakaishi katika hali ileile waliyoishi wakati walipokuwa chini ya utawala wa mfalme Daudi na mfalme Solomoni.

18. Rehoboamu alioa mke, jina lake Mahalathi binti Yeremothi mwana wa Daudi. Mama yake alikuwa Abihaili binti Eliabu, mwana wa Yese.

Kusoma sura kamili 2 Mambo Ya Nyakati 11