Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wafalme 9:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Mfalme Solomoni alipomaliza kujenga nyumba ya Mwenyezi-Mungu na ikulu na majengo mengine yote aliyokusudia kujenga,

2. Mwenyezi-Mungu alimtokea tena kama alivyomtokea kule Gibeoni.

3. Mwenyezi-Mungu alimwambia, “Nimesikia sala yako na ombi lako. Nimeitakasa nyumba hii ambayo umenijengea ili watu waliabudu jina langu hapa milele. Nitaichunga na kuipenda wakati wote.

4. Nawe kama ukinitumikia kwa unyofu wa moyo na uadilifu kama baba yako Daudi alivyofanya, ukitii amri zangu na kutimiza yale yote niliyokuamuru, ukifuata masharti yangu na maagizo yangu;

5. basi, mimi nitakiimarisha kiti chako cha kifalme juu ya Israeli milele, kama nilivyomwahidi Daudi baba yako, nikisema, Hutakosa mtu wa kukaa juu ya kiti cha enzi cha Israeli.

6. Lakini wewe au watoto wako mkigeuka na kuacha kunifuata, msiposhika amri zangu na maongozi niliyowapani, mkienda kutumikia miungu mingine na kuiabudu,

7. basi, nitawahamisha watu wangu, Israeli, kutoka nchi hii ambayo nimewapa; kadhalika na nyumba hii ambayo nimeiweka wakfu kwa ajili ya jina langu, nitaitupilia mbali nami, na kuifanya kitu cha kupuuzwa na kudharauliwa miongoni mwa mataifa yote.

8. Na nyumba hii itabomoka na kuwa magofu; kila apitaye karibu atashtuka na kutikisa kichwa, na kuuliza, ‘Kwa nini Mwenyezi-Mungu amefanya hivyo kwa nchi hii na kwa nyumba hii?’

9. Watu wengine watajibu, ‘Ni kwa sababu walimwacha Mwenyezi-Mungu, Mungu wao, aliyewatoa babu zao katika nchi ya Misri, wakashikamana na miungu mingine, wakaiabudu na kuitumikia; kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu amewaletea maafa haya yote.’”

10. Kisha miaka ishirini ilipokwisha pita, ambayo Solomoni alizijenga zile nyumba mbili: Nyumba ya Mwenyezi-Mungu na ikulu,

11. mfalme Solomoni alimpa Hiramu mfalme wa Tiro, miji ishirini katika mkoa wa Galilaya (kwa sababu huyo Hiramu alikuwa amempelekea Solomoni mbao za mierezi na miberoshi, na dhahabu pia, kadiri alivyohitaji kwa ujenzi).

12. Lakini Hiramu alipowasili kutoka Tiro na kuiona miji hiyo aliyokuwa amepewa na Solomoni hakupendezwa nayo.

13. Basi, akamwuliza Solomoni, “Ndugu yangu, ni miji gani hii ambayo umenipa?” Ndio sababu miji hiyo inaitwa nchi ya Kabuli hata leo.

Kusoma sura kamili 1 Wafalme 9