Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wafalme 8:47-61 Biblia Habari Njema (BHN)

47. kama watakapokuwa huko uhamishoni watajirudi moyoni na kutubu na kukuomba msamaha, wakisema, ‘Tumetenda dhambi; tumepotoka na kufanya maovu;’

48. pia wakati huo watakapokuwa katika nchi ya adui zao, wakitubu kwa moyo wao wote na kwa roho yao yote, na kama watakuomba wakielekea nchi yao ambayo uliwapatia babu zao, wakielekea mji huu ambao uliuchagua na nyumba hii ambayo nimeijenga kwa ajili ya jina lako,

49. basi, nakusihi kutoka huko mbinguni uliko usikie sala yao na ombi lao uwapatie haki zao.

50. Uwasamehe watu wako dhambi walizotenda dhidi yako na uasi wao, uwahurumie mbele ya adui zao, ili nao wapate kuwahurumia,

51. maana ni watu wako, na ni mali yako; watu ambao uliwatoa Misri kutoka katika tanuri ya chuma.

52. “Uangalie ombi la mtumishi wako na ombi la watu wako, Israeli, uwasikie kila wanapokuomba.

53. Kwa sababu, ee Bwana Mwenyezi-Mungu uliwatenga na watu wa mataifa mengine duniani, ili wawe mali yako – kama ulivyotangaza kwa njia ya Mose, mtumishi wako, wakati ule ulipowatoa babu zetu katika nchi ya Misri.”

54. Solomoni alipomaliza kusema sala hiyo yote na ombi lake kwa Mwenyezi-Mungu aliinuka kutoka pale mbele ya madhabahu ya Mwenyezi-Mungu, mahali alipokuwa amepiga magoti akiinua mikono yake juu.

55. Alisimama, akawabariki Waisraeli wote waliokuwa wamekusanyika hapo, akisema kwa sauti kubwa,

56. “Atukuzwe Mwenyezi-Mungu ambaye amewapatia starehe watu wake Israeli, kulingana na ahadi yake. Ametimiza ahadi zake zote njema alizozitoa kupitia kwa mtumishi wake Mose.

57. Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, awe nasi, kama alivyokuwa na babu zetu; tunaomba asituache, wala asitutupe.

58. Yeye aelekeze mioyo yetu kwake, ili tufuate njia zake, tukishika amri zake, maongozi yake na maagizo yake aliyowapa babu zetu.

59. Basi, maneno yangu haya ambayo ni ombi langu mbele ya Mwenyezi-Mungu, yawe karibu na Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, mchana na usiku, naye amjalie mtumishi wake, na watu wake Israeli, ili wafanikiwe katika haja zao za kila siku.

60. Nayo mataifa yote ulimwenguni yatajua kwamba kweli Mwenyezi-Mungu ndiye Mungu; wala hakuna mwingine.

61. Nanyi, muwe waaminifu kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu, mkifuata masharti yake na kutii amri zake zote kama mnavyofanya hivi leo.”

Kusoma sura kamili 1 Wafalme 8