Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wafalme 8:46-56 Biblia Habari Njema (BHN)

46. “Ikiwa watatenda dhambi dhidi yako maana hakuna mtu asiyetenda dhambi, nawe ukiwakasirikia na kuwaacha washindwe na adui, hata wapelekwe mateka mpaka nchi ya adui iliyoko mbali au karibu;

47. kama watakapokuwa huko uhamishoni watajirudi moyoni na kutubu na kukuomba msamaha, wakisema, ‘Tumetenda dhambi; tumepotoka na kufanya maovu;’

48. pia wakati huo watakapokuwa katika nchi ya adui zao, wakitubu kwa moyo wao wote na kwa roho yao yote, na kama watakuomba wakielekea nchi yao ambayo uliwapatia babu zao, wakielekea mji huu ambao uliuchagua na nyumba hii ambayo nimeijenga kwa ajili ya jina lako,

49. basi, nakusihi kutoka huko mbinguni uliko usikie sala yao na ombi lao uwapatie haki zao.

50. Uwasamehe watu wako dhambi walizotenda dhidi yako na uasi wao, uwahurumie mbele ya adui zao, ili nao wapate kuwahurumia,

51. maana ni watu wako, na ni mali yako; watu ambao uliwatoa Misri kutoka katika tanuri ya chuma.

52. “Uangalie ombi la mtumishi wako na ombi la watu wako, Israeli, uwasikie kila wanapokuomba.

53. Kwa sababu, ee Bwana Mwenyezi-Mungu uliwatenga na watu wa mataifa mengine duniani, ili wawe mali yako – kama ulivyotangaza kwa njia ya Mose, mtumishi wako, wakati ule ulipowatoa babu zetu katika nchi ya Misri.”

54. Solomoni alipomaliza kusema sala hiyo yote na ombi lake kwa Mwenyezi-Mungu aliinuka kutoka pale mbele ya madhabahu ya Mwenyezi-Mungu, mahali alipokuwa amepiga magoti akiinua mikono yake juu.

55. Alisimama, akawabariki Waisraeli wote waliokuwa wamekusanyika hapo, akisema kwa sauti kubwa,

56. “Atukuzwe Mwenyezi-Mungu ambaye amewapatia starehe watu wake Israeli, kulingana na ahadi yake. Ametimiza ahadi zake zote njema alizozitoa kupitia kwa mtumishi wake Mose.

Kusoma sura kamili 1 Wafalme 8