Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wafalme 8:33-45 Biblia Habari Njema (BHN)

33. “Ikiwa watu wako Waisraeli, wameshindwa na adui zao kwa sababu ya dhambi walizotenda dhidi yako, nao wakitubu kwako na kulikiri jina lako, wakiomba msamaha wako kwa unyenyekevu katika nyumba hii,

34. basi, uwasikie kutoka huko mbinguni, uwasamehe watu wako Israeli dhambi zao, halafu uwarudishe katika nchi uliyowapa babu zao.

35. “Mvua isiponyesha kwa sababu wametenda dhambi dhidi yako, wakiomba wakielekea mahali hapa na kulikiri jina lako, pia wakiziacha dhambi zao unapowaonya,

36. tafadhali, uwasikie kutoka huko mbinguni, na usamehe dhambi za watumishi wako, watu wako Israeli, huku ukiwafundisha kufuata njia nyofu; ukanyeshe mvua katika nchi yako hii ambayo uliwapa watu wako iwe mali yako.

37. “Iwapo kuna njaa nchini, au tauni, ukame, ugonjwa wa mimea, nzige au viwavi; au ikiwa watu wako wamezingirwa na adui zao katika mji wao wowote ule; ikiwa kuna pigo lolote au ugonjwa wowote,

38. tafadhali, usikie maombi yoyote yatakayoombwa na watu wako, Israeli, au yatakayoombwa na mtu yeyote au watu wako wote wa Israeli; kila mtu akijua taabu za moyoni mwake, akikuomba huku akinyosha mikono yake kuelekea kwenye nyumba hii.

39. Basi, usikie huko kwako mbinguni, utoe msamaha na kuchukua hatua; pia umtendee kila mtu kadiri anavyostahili (kwani ni wewe tu ujuaye mawazo ya mioyo ya wanadamu wote);

40. ili wakutii wakati wote wanapoishi katika nchi uliyowapa babu zetu.

41. “Vivyo hivyo, wakati mgeni asiye mmoja wa watu wako Israeli akija kutoka nchi ya mbali kwa ajili ya jina lako

42. (maana watu wa mataifa mengine watasikia sifa zako na kuhusu nguvu na uwezo wako), mtu huyo akija na kuomba katika nyumba hii,

43. nakusihi umsikie kutoka huko mbinguni, na umjalie huyo mgeni yote atakayokuomba; kusudi watu wote ulimwenguni wapate kujua jina lako na kukutii kama wafanyavyo watu wako, Israeli, na wapate kufahamu kwamba nyumba hii ambayo nimeijenga, inajulikana kwa jina lako.

44. “Watu wako wakienda vitani kupigana na adui yao kokote kule utakakowapeleka, nao wakikuomba wakielekea mji uliouchagua na nyumba niliyoijenga kwa ajili ya jina lako,

45. nakusihi usikie sala yao na maombi yao huko mbinguni, uwapatie ushindi vitani.

Kusoma sura kamili 1 Wafalme 8