Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wafalme 22:33-45 Biblia Habari Njema (BHN)

33. Makapteni walipotambua kwamba hakuwa mfalme wa Israeli waliacha kumshambulia, wakarudi.

34. Lakini, askari mmoja wa Aramu, akauvuta upinde wake kwa kubahatisha, mshale ukamchoma mfalme wa Israeli mahali pa kuungana mavazi yake ya chuma kifuani. Ahabu akamwambia dereva wa gari lake, “Geuza gari uniondoe vitani. Nimejeruhiwa!”

35. Na mapigano siku hiyo yakazidi kuwa makali, huku mfalme ameegemeshwa garini, anawaelekea watu wa Aramu. Ilipofika jioni, akafariki. Damu ikawa inamtoka jerahani mwake na kutiririka hadi chini ya gari.

36. Mnamo machweo ya jua, amri ikatolewa: “Kila mtu arudi mjini kwake; kila mtu arudi nchini kwake!”

37. Mfalme Ahabu alipofariki maiti yake ilipelekwa Samaria, ikazikwa huko.

38. Gari lake la kukokotwa waliliosha katika bwawa la Samaria, mbwa wakairamba damu yake, nao makahaba wakaoga humo, sawa kabisa na neno alilosema Mwenyezi-Mungu.

39. Matendo mengine ya mfalme Ahabu, jinsi alivyojenga na kupamba nyumba yake kwa pembe, na miji yote aliyojenga, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Israeli.

40. Ahabu alipofariki, mwanawe Ahazia alitawala mahali pake.

41. Mnamo mwaka wa nne wa utawala wa mfalme Ahabu wa Israeli, Yehoshafati mwana wa Asa, alianza kutawala Yuda.

42. Yehoshafati alikuwa na umri wa miaka thelathini na mitano alipoanza kutawala. Alitawala kutoka Yerusalemu kwa muda wa miaka ishirini na mitano. Mama yake alikuwa Azuba binti Shilhi.

43. Alitenda mema mbele ya Mwenyezi-Mungu kama alivyofanya baba yake Asa.

44. Lakini hakupaharibu mahali pa kutambikia vilimani. Watu waliendelea kutambikia na kufukiza ubani mahali hapo.

45. Yehoshafati pia, alifanya mapatano ya amani na mfalme wa Israeli.

Kusoma sura kamili 1 Wafalme 22