Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wafalme 21:1-16 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Nabothi, mwenyeji wa Yezreeli, alikuwa na shamba lake la mizabibu huko Yezreeli, karibu na ikulu ya Ahabu, mfalme wa Samaria.

2. Basi, siku moja, Ahabu akamwambia Nabothi, “Nipe shamba lako la mizabibu nilifanye shamba la mboga, kwa sababu liko karibu na nyumba yangu. Nitakupa shamba lingine zuri zaidi, au ukitaka, nitakulipa thamani yake, fedha taslimu.”

3. Lakini, Nabothi akamjibu, “Jambo la kukupa wewe urithi nilioupata kwa wazee wangu, Mwenyezi-Mungu na apishe mbali.”

4. Hapo, Ahabu akaenda zake nyumbani amejaa chuki na huzuni nyingi, kwa sababu Nabothi, mwenyeji wa Yezreeli, alimwambia kwamba hatampa kile alichorithi kutoka kwa wazee wake. Basi, akajilaza kitandani, akauficha uso wake na kususia chakula.

5. Yezebeli, mkewe, akamwendea na kumwuliza, “Mbona umejaa huzuni moyoni hata kula huli?”

6. Naye akamwambia, “Kwa sababu nilizungumza na Nabothi, mwenyeji wa Yezreeli, nikamtaka aniuzie shamba lake la mizabibu, ama akipenda nimpe shamba lingine badala ya hilo. Lakini yeye akaniambia, ‘Sitakupa shamba langu la mizabibu.’”

7. Hapo, Yezebeli, mkewe, akamwambia, “Anayetawala Israeli ni nani? Si ni wewe? Amka, ule na uchangamke; mimi binafsi nitakupa shamba la mizabibu la Nabothi, Myezreeli.”

8. Basi, Yezebeli akaandika barua kadha kwa jina la Ahabu na kuzipiga mhuri wa mfalme. Kisha akapeleka barua hizo kwa wazee na watu mashuhuri walioishi na Nabothi huko mjini.

9. Barua zenyewe ziliandikwa hivi: “Pigeni mbiu ya mfungo, mkutane na kumpa Nabothi mahali pa heshima kati ya watu.

10. Kisha, tafuteni walaghai wawili wamkabili na kumshtaki wakisema: ‘Wewe umemwapiza Mungu na mfalme.’ Kisha mtoeni nje, mkamuue kwa kumpiga mawe!”

11. Basi, wakazi wenzake Nabothi, wazee na watu mashuhuri wa mji wa Yezreeli, wakafanya kama Yezebeli alivyowaagiza. Kwa mujibu wa barua aliyowapelekea,

12. wakapiga mbiu ya mfungo, wakakutana na kumweka Nabothi mahali pa heshima kati ya watu.

13. Wale walaghai wawili wakaketi kumkabili Nabothi, kisha wakamshtaki hadharani wakisema, “Nabothi amemwapiza Mungu na mfalme.” Basi, Nabothi akatolewa nje ya mji, akauawa kwa kupigwa mawe.

14. Kisha, Yezebeli akapelekewa habari kwamba Nabothi amekwisha uawa kwa kupigwa mawe.

15. Mara tu Yezebeli alipopata habari kwamba Nabothi amekwisha uawa kwa kupigwa mawe, akamwambia Ahabu, “Inuka! Nenda ukamiliki lile shamba la mizabibu la Nabothi, Myezreeli, ambalo alikataa kukuuzia. Nabothi hayuko hai tena; amekwisha fariki.”

16. Mara tu Ahabu aliposikia Nabothi amekwisha fariki, aliinuka kwenda kulimiliki shamba la mizabibu la Nabothi.

Kusoma sura kamili 1 Wafalme 21