Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wafalme 16:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Yehu mwana wa Hanani, dhidi ya Baasha:

2. “Wewe Baasha, mimi nilikuinua kutoka mavumbini, nikakufanya kiongozi wa watu wangu Israeli. Wewe umemwiga Yeroboamu, ukawafanya watu wangu Israeli watende dhambi na kunikasirisha kwa dhambi zao.

3. Haya! Sasa, nitakufutilia mbali wewe na jamaa yako; nitaitendea jamaa yako kama nilivyoitendea jamaa ya Yeroboamu mwana wa Nebati.

4. Yeyote wa jamaa yako atakayefia mjini, mbwa watamla; na yeyote atakayefia shambani, ndege wa angani watamla.”

5. Matendo mengine ya Baasha na ushujaa wake, yote yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Israeli.

6. Hatimaye, Baasha alifariki, akazikwa huko Tirza; mwanawe Ela akatawala mahali pake.

7. Tena neno la Mwenyezi-Mungu dhidi ya Baasha na jamaa yake, lilimjia Yehu mwanawe Hanani kwa sababu ya maovu aliyotenda mbele ya Mwenyezi-Mungu. Baasha alimkasirisha Mwenyezi-Mungu kwa matendo yake; alimwiga Yeroboamu na jamaa yake na kuiletea jamaa yake maangamizi.

8. Mnamo mwaka wa ishirini na sita wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda, Ela mwana wa Baasha, alianza kutawala huko Israeli kutoka Tirza. Alitawala kwa muda wa miaka miwili.

9. Mtumishi wake Zimri ambaye alisimamia nusu ya kikosi cha magari yake ya kukokotwa, alikula njama juu yake. Siku moja, mfalme Ela alipokuwa huko Tirza nyumbani kwa Arsa aliyekuwa msimamizi wa ikulu, alikunywa, akalewa.

10. Basi, Zimri akaingia ndani, akamuua. Kisha akatawala mahali pake. Huu ulikuwa mwaka wa ishirini na saba wa utawala wa Asa mfalme wa Yuda.

11. Mara tu alipoanza kutawala, Zimri aliwaua watu wote wa jamaa ya Baasha; hakumwachia hata mwanamume mmoja wa jamaa yake wala wa rafiki zake;

12. ikawa kama alivyosema Mwenyezi-Mungu dhidi ya Baasha, kwa njia ya nabii Yehu.

Kusoma sura kamili 1 Wafalme 16