Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wafalme 14:21-31 Biblia Habari Njema (BHN)

21. Rehoboamu, mwanawe Solomoni, alikuwa na umri wa miaka arubaini na mmoja alipoanza kutawala Yuda. Naye alitawala kwa muda wa miaka kumi na saba katika Yerusalemu, mji ambao Mwenyezi-Mungu aliuchagua miongoni mwa miji ya makabila yote ya Israeli aabudiwe humo. Mama yake Rehoboamu alikuwa Naama kutoka Amoni.

22. Watu wa Yuda walitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu. Walimkasirisha kwa dhambi zao walizotenda, nyingi kuliko za babu zao.

23. Walijitengenezea pia mahali pa ibada, minara ya kutambikia, na sanamu za Ashera, juu ya kila kilima kirefu na chini ya kila mti wenye majani mabichi.

24. Tena, kukawa na ibada za ukahaba nchini; watu walitenda matendo ya kuchukiza ya mataifa ambayo Mungu aliyafukuza Waisraeli walipokuwa wanaingia nchini Kanaani.

25. Katika mwaka wa tano wa utawala wa Rehoboamu, Shishaki mfalme wa Misri, aliushambulia mji wa Yerusalemu,

26. akaichukua hazina yote ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu na ya ikulu; alichukua kila kitu; pia alichukua ngao zote za dhahabu alizozitengeneza Solomoni.

27. Badala ya ngao hizo, mfalme Rehoboamu alitengeneza ngao za shaba na kuziweka chini ya ulinzi wa wangojamlango wa ikulu.

28. Kila wakati mfalme alipokwenda katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, walinzi walizibeba ngao hizo, na baadaye wakazirudisha katika chumba cha ulinzi.

29. Matendo mengine ya mfalme Rehoboamu, na yote aliyoyafanya, yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati ya Wafalme wa Yuda.

30. Daima kulikuwako vita kati ya Rehoboamu na Yeroboamu.

31. Hatimaye, Rehoboamu alifariki na kuzikwa kwenye makaburi ya wazee wake, katika mji wa Daudi. Mama yake aliitwa Naama kutoka Amoni, na Abiyamu mwanawe akatawala mahali pake.

Kusoma sura kamili 1 Wafalme 14