Agano la Kale

Agano Jipya

1 Samueli 20:24-36 Biblia Habari Njema (BHN)

24. Basi, Daudi akajificha shambani. Wakati wa sherehe za mwezi mwandamo, mfalme Shauli akaketi mezani kula.

25. Kama ilivyokuwa kawaida yake, mfalme aliketi kwenye kiti chake kilichokuwa karibu ukutani. Yonathani akaketi mkabala na mfalme na Abneri akaketi karibu na mfalme. Lakini mahali pa Daudi pakawa wazi.

26. Siku hiyo, Shauli hakusema lolote, kwani alifikiri kuwa labda Daudi amepatwa na tatizo au yeye si safi kuhudhuria sherehe hiyo.

27. Siku ya pili, baada ya sherehe za mwezi mwandamo, bado mahali pa Daudi palikuwa wazi. Shauli akamwuliza mwanawe Yonathani, “Kwa nini Daudi mwana wa Yese, hakuja kwenye chakula, jana na leo?”

28. Yonathani akamjibu, “Alinisihi sana nimruhusu aende Bethlehemu.

29. Aliniambia, ‘Niruhusu niende kwa jamaa yangu, kwa kuwa wanafanya karamu ya tambiko huko mjini, na ndugu yangu amenitaka niwepo. Hivyo kama ni sawa kwako niruhusu niende kwa ndugu zangu’. Ndio maana hayuko hapa kushiriki chakula cha mfalme.”

30. Hapo Shauli akawaka hasira dhidi ya Yonathani, akamwambia, “Mwana wa mwanamke mpotovu na mwasi wewe! Ninajua kuwa umejichagulia mwana wa Yese kwa aibu yako mwenyewe, na kumwaibisha mama yako!

31. Je, hujui kwamba Daudi awapo hai, wewe hutaweza kupata fursa ya kuwa mfalme wa nchi hii? Sasa nenda ukamlete hapa kwangu, kwa kuwa lazima auawe.”

32. Yonathani akamjibu, “Kwa nini auawe? Amefanya nini?”

33. Lakini Shauli mara akamtupia Yonathani mkuki ili amuue. Naye Yonathani akatambua kuwa baba yake alikuwa amepania kumwua Daudi.

34. Hapo Yonathani, huku akiwa amekasirika sana, aliondoka mezani kwa haraka, wala hakula chakula chochote siku hiyo ya pili ya sherehe za mwezi mwandamo. Yonathani alihuzunika sana juu ya Daudi kwa sababu baba yake alikuwa amemwaibisha.

35. Kesho yake asubuhi, Yonathani alikwenda kule shambani, kukutana na Daudi kama walivyoagana. Alikwenda huko na kijana mmoja wa kiume.

36. Alipofika huko alimwambia yule kijana wake, “Kimbia ukaitafute mishale ambayo nitapiga.” Yule kijana alipokuwa anakimbia, Yonathani akapiga mshale mbele yake.

Kusoma sura kamili 1 Samueli 20