Agano la Kale

Agano Jipya

1 Samueli 20:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Daudi alikimbia kutoka Nayothi katika Rama, akaenda mpaka kwa Yonathani, akamwambia, “Nimefanya nini? Kosa langu ni nini? Nimemtendea baba yako dhambi gani hata ajaribu kuyaangamiza maisha yangu?”

2. Yonathani akamjibu, “Hilo na liwe mbali nawe. Hutakufa. Baba yangu hafanyi jambo lolote, liwe kubwa au dogo, bila ya kunieleza. Hata jambo hili hawezi kunificha. Sivyo ilivyo hata kidogo.”

3. Daudi akaapa pia, “Hakika baba yako anajua vizuri unavyonipenda; na anafikiri kukuficha juu ya jambo hili ili usihuzunike atakapolitenda. Lakini, kwa vyovyote vile, naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai, nawe ulivyo hai, kwamba kati yangu na mauti ipo hatua moja tu!”

4. Yonathani akamwambia, “Lolote utakalosema nitakutendea.”

5. Daudi akamwambia, “Kesho ni sherehe za mwezi mwandamo, nami natazamiwa kuwapo mezani kula pamoja na mfalme. Lakini niache, nikajifiche huko shambani hadi siku ya tatu jioni.

6. Baba yako akinikosa mezani kwa chakula, akauliza habari zangu, basi mwambie, ‘Daudi amenisihi nimpe ruhusa ili aende mjini kwake Bethlehemu, kuhudhuria tambiko ya kila mwaka pamoja na jamaa yake’.

7. Ikiwa ataona hilo ni sawa, basi, ujue kuwa mambo yangu, mimi mtumishi wako, yako sawa. La sivyo, kusudi lake juu yangu ni baya.

8. Hivyo nifanyie kwa hisani yako kwani umefanya agano takatifu nami, mimi mtumishi wako, mbele ya Mwenyezi-Mungu. Lakini, kama nimefanya kosa basi, na uniue wewe mwenyewe; kwa nini unipeleke kwa baba yako ili aniue?”

9. Yonathani akamjibu, “Wazo hilo na liwe mbali nawe. Hakika, kama ningejua kuwa baba yangu amekusudia mabaya juu yako nisingekuficha.”

10. Daudi akauliza, “Nitajuaje ikiwa baba yako atakujibu kwa ukali?”

11. Yonathani akamjibu, “Njoo twende shambani!” Basi, wakaenda.

Kusoma sura kamili 1 Samueli 20