Agano la Kale

Agano Jipya

1 Samueli 2:19-30 Biblia Habari Njema (BHN)

19. Kila mwaka mama yake alimfumia vazi dogo, na kumpelekea alipokuwa akienda na mumewe kutolea tambiko ya kila mwaka.

20. Eli aliwabariki Elkana na mkewe, akisema, “Mwenyezi-Mungu na akupe wewe Elkana watoto wengine kwa mwanamke huyu ili wachukue mahali pa yule uliyempa Mwenyezi-Mungu.” Kisha wao hurudi nyumbani.

21. Mwenyezi-Mungu alimhurumia Hana naye akajaliwa kupata watoto wa kiume watatu na mabinti wawili. Mtoto Samueli akaendelea kukua mbele ya Mwenyezi-Mungu.

22. Wakati huo Eli alikuwa mzee sana. Aliposikia yote ambayo watoto wake wa kiume walikuwa wanawatendea Waisraeli, jinsi walivyokuwa wanalala na wanawake waliokuwa wanahudumu kwenye mlango wa hema la mkutano,

23. aliwauliza, “Kwa nini mnafanya mambo haya? Nasikia kutoka kwa watu wote juu ya maovu mnayoyafanya.

24. Msifanye hivyo wanangu kwa sababu mambo hayo ninayoyasikia kutoka kwa watu wa Mwenyezi-Mungu ni mabaya.

25. Mtu akimkosea mwenzake, anaweza kuombewa kwa Mungu, ili Mungu amsamehe. Lakini mtu akimkosea Mwenyezi-Mungu nani awezaye kumwombea msamaha?” Lakini watoto hao hawakumsikiliza baba yao, kwani Mwenyezi-Mungu alikwisha kata shauri kuwaua.

26. Mtoto Samueli aliendelea kukua, akazidi kupendwa na Mwenyezi-Mungu na watu.

27. Siku moja, mtu wa Mungu alimwendea Eli, akamwambia, “Mwenyezi-Mungu amesema hivi: ‘Nilijijulisha kwa jamaa ya Aroni, wazee wako, walipokuwa watumwa wa Farao nchini Misri.

28. Kati ya makabila yote ya Israeli nilimchagua Aroni na jamaa yake kuwa makuhani wangu, wanitumikie madhabahuni, wafukize ubani na kuvaa kizibao mbele yangu. Nikaipatia jamaa ya mzee wako tambiko zangu ambazo Waisraeli walinitolea kwa moto.

29. Kwa nini basi, umezionea wivu tambiko na sadaka nilizowaamuru watu waniletee? Wewe umewastahi watoto wako kuliko mimi kwa kujinenepesha nyinyi wenyewe kwa kula sehemu nzurinzuri za sadaka ambazo watu wangu wa Israeli hunitolea!’

30. Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, anatamka hivi, ‘Niliahidi kwamba jamaa yako na jamaa ya wazee wako mtakuja mbele yangu kunitumikia milele;’ lakini sasa Mwenyezi-Mungu anakutangazia hivi, ‘Jambo hilo liwe mbali nami.’ Nitawaheshimu wale wanaoniheshimu, na wale wanaonidharau, nitawadharau.

Kusoma sura kamili 1 Samueli 2