Agano la Kale

Agano Jipya

1 Samueli 16:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Mwenyezi-Mungu akamwambia Samueli, “Utamlilia Shauli mpaka lini? Wewe unajua kuwa mimi nimemkataa kuwa mfalme juu ya Israeli. Sasa, jaza upembe wako mafuta, uondoke. Nitakutuma kwa Yese wa mji wa Bethlehemu. Maana nimejipatia mfalme miongoni mwa wanawe.”

2. Samueli akasema, “Nitawezaje kwenda? Kama Shauli akisikia habari hizo, ataniua!” Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Chukua ndama pamoja nawe, na ukifika huko useme, ‘Nimekuja kumtolea Mwenyezi-Mungu tambiko’.

3. Mwalike Yese kwenye tambiko hiyo nami nitakuonesha la kufanya. Utampaka mafuta kwa ajili yangu mtu yule nitakayekutajia.”

4. Samueli akafanya kama alivyoambiwa na Mwenyezi-Mungu, akaenda Bethlehemu. Wazee wa mji wakatoka kumlaki wakiwa wanatetemeka, wakamwuliza, “Je, umekuja kwa amani?”

5. Samueli akawaambia, “Nimekuja kwa amani. Nimekuja kumtolea tambiko Mwenyezi-Mungu. Jitakaseni wenyewe halafu twendeni kutoa tambiko.” Samueli akamtakasa Yese pamoja na wanawe, akawakaribisha kwenye tambiko.

6. Walipofika, na Samueli alipomwona Eliabu, alijisemea moyoni mwake, “Hakika, mpakwa mafuta wa Mwenyezi-Mungu ndiye huyu aliye mbele ya Mwenyezi-Mungu!”

7. Lakini Mwenyezi-Mungu alimwambia, “Usiangalie sura yake na urefu wa kimo chake. Mimi nimemkataa kwani siangalii mambo kama wanavyoyaangalia binadamu wenye kufa. Binadamu huangalia uzuri wa nje, lakini mimi naangalia moyoni.”

Kusoma sura kamili 1 Samueli 16