Agano la Kale

Agano Jipya

1 Samueli 10:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Ndipo Samueli akachukua chupa ndogo ya mafuta akammiminia Shauli kichwani, akambusu na kumwambia, “Mwenyezi-Mungu amekutia mafuta uwe mtawala juu ya watu wake.

2. Leo tutakapoagana, utakutana na watu wawili karibu na kaburi la Raheli huko Selsa katika nchi ya Benyamini. Hao watakuambia kuwa wale punda uliokuwa unawatafuta wamekwisha patikana. Baba yako ameacha kufikiri juu ya punda, ila ana wasiwasi juu yako, akijiuliza kila mara, ‘Nitafanya nini juu ya mwanangu?’

3. Kutoka hapo utakwenda kwenye mwaloni wa Tabori, mahali ambapo utakutana na wanaume watatu wakiwa njiani kwenda kumtolea Mungu tambiko, huko Betheli. Mmoja wao atakuwa anawachukua wanambuzi watatu, wa pili atakuwa anachukua mikate mitatu na wa tatu atakuwa amebeba kiriba cha divai.

4. “Watakusalimia na kukupa mikate miwili, nawe utaipokea mikononi mwao.

5. Kisha, utakapofika huko Gibea-elohimu, mahali ambapo pana kambi ya kijeshi ya Wafilisti; hapo, utakapokuwa unakaribia mji, utakutana na kundi la manabii. Manabii hao watakuwa wanatoka mahali pa juu huku wakipiga vinubi, matari, filimbi na zeze, na watakuwa wanatabiri.

6. Roho ya Mwenyezi-Mungu itakujia kwa nguvu, nawe utaanza kutabiri pamoja nao na kugeuka kuwa mtu mwingine.

7. Wakati mambo haya yatakapokutokea, chochote utakachoweza kufanya kifanye, kwani Mungu yu pamoja nawe.

8. Utanitangulia kwenda mjini Gilgali, mahali ambapo nitakukuta na kutoa sadaka ya kuteketezwa na tambiko za amani. Utaningojea hapo kwa muda wa siku saba mpaka nije na kukuonesha la kufanya.”

9. Shauli alipogeuka ili kumwacha Samueli, Mungu akabadili moyo wa Shauli. Yale yote aliyoambiwa na Samueli yakatokea siku hiyo.

10. Shauli na mtumishi wake walipofika huko Gibea, alilakiwa na kundi la manabii. Roho ya Mungu ilimjia kwa nguvu, na Shauli akaanza kutabiri pamoja na manabii hao.

Kusoma sura kamili 1 Samueli 10