Agano la Kale

Agano Jipya

1 Samueli 1:9-24 Biblia Habari Njema (BHN)

9. Siku moja, walipokuwa wamemaliza kula na kunywa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu huko Shilo, Hana akasimama. Wakati huo, kuhani Eli alikuwa amekaa kwenye kiti karibu na mwimo wa nyumba ya Mwenyezi-Mungu.

10. Hana alikuwa na huzuni sana. Na alipokuwa anamwomba Mwenyezi-Mungu akawa analia kwa uchungu.

11. Akaweka nadhiri akisema, “Ee Mwenyezi-Mungu wa majeshi, kama tu utayaangalia mateso yangu mimi mtumishi wako ukanikumbuka mimi, bila kunisahau, mimi mtumishi wako, ukanijalia mimi mtumishi wako, mtoto wa kiume, nitakupa wewe Mwenyezi-Mungu mtoto huyo awe wako maisha yake yote; wembe hautapita kichwani pake kamwe.”

12. Hana aliendelea kumwomba Mwenyezi-Mungu kwa muda mrefu, na kuhani Eli akawa anaangalia midomo yake.

13. Hana alikuwa akiomba kimoyomoyo, lakini midomo yake ilikuwa inachezacheza, ila sauti yake haikusikika. Hivyo Eli akafikiri kuwa Hana amelewa.

14. Kwa hiyo Eli akamwambia, “Utaendelea kulewa hadi lini? Achana na kunywa divai.”

15. Lakini Hana akamjibu, “Sivyo bwana wangu; mimi ni mwanamke mwenye taabu mno; mimi sijanywa divai wala kinywaji kikali, bali nimekuwa nikimtolea Mwenyezi-Mungu yaliyomo rohoni mwangu.

16. Usinidhanie kuwa mimi ni mwanamke asiyefaa kitu. Kwa muda wote huu nimekuwa nikisema mahangaiko yangu na taabu yangu.”

17. Ndipo Eli akamwambia, “Nenda kwa amani; naye Mungu wa Israeli akupe kile ulichomwomba.”

18. Hana akasema, “Naomba nami mtumishi wako nipate kibali mbele yako.” Hana akaenda zake, akala chakula na hakuwa na huzuni tena.

19. Kesho yake asubuhi, Elkana na jamaa yake waliamka asubuhi na mapema, na baada ya kumwabudu Mwenyezi-Mungu, walirudi nyumbani Rama. Elkana akalala na mkewe Hana, naye Mwenyezi-Mungu akamkumbuka.

20. Hivyo Hana akapata mimba, akajifungua mtoto wa kiume. Hana akamwita mtoto huyo Samueli, kwani alisema, “Nimemwomba kwa Mwenyezi-Mungu.”

21. Elkana na jamaa yake yote wakaenda tena Shilo na kumtolea Mwenyezi-Mungu tambiko ya kila mwaka na kutimiza nadhiri.

22. Lakini safari hii Hana hakwenda, kwani alimwambia hivi mumewe, “Mara mtoto atakapoachishwa kunyonya, nitampeleka ili awekwe mbele ya Mwenyezi-Mungu, abaki huko daima.”

23. Elkana, mumewe, akamjibu, “Fanya unaloona linafaa. Ngojea hadi utakapomwachisha mtoto kunyonya. Mwenyezi-Mungu aifanye nadhiri yako kuwa kweli.” Basi, Hana alibaki nyumbani, akaendelea kumlea mtoto wake hadi alipomwachisha kunyonya.

24. Alipomwachisha kunyonya alimpeleka pamoja na fahali wa miaka mitatu, gunia la unga na kiriba cha divai. Hana alimwingiza mtoto kwenye nyumba ya Mwenyezi-Mungu huko Shilo, naye mtoto alikuwa mdogo tu.

Kusoma sura kamili 1 Samueli 1