Agano la Kale

Agano Jipya

Matendo 12:3-11 Biblia Habari Njema (BHN)

3. Alipoona kuwa kitendo hicho kiliwapendeza Wayahudi, aliendelea, akamkamata Petro. (Hiyo ilifanyika wakati wa sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu).

4. Baada ya kutiwa nguvuni, Petro alifungwa gerezani, akawekwa chini ya ulinzi wa vikundi vinne vya askari wannewanne. Herode alikusudia kumtoa hadharani baada ya sikukuu ya Pasaka.

5. Basi, Petro alipokuwa gerezani, kanisa lilikuwa linamwombea kwa Mungu kwa moyo.

6. Usiku, kabla ya siku ile ambayo Herode angemtoa Petro hadharani, Petro alikuwa amelala kati ya askari wawili. Alikuwa amefungwa minyororo miwili, na walinzi walikuwa wanalinda lango la gereza.

7. Ghafla, malaika wa Bwana akasimama karibu naye na mwanga ukaangaza kile chumba cha gereza. Malaika akamgusa ubavuni akamwamsha akisema, “Ondoka upesi!” Mara ile minyororo iliyomfunga mikono ikakatika na kuanguka chini.

8. Malaika akamwambia, “Jifunge mshipi wako, vaa viatu vyako.” Akafanya hivyo. Kisha huyo malaika akamwambia, “Vaa koti lako, unifuate.”

9. Petro akamfuata nje lakini hakujua kama hayo yaliyofanywa na huyo malaika yalikuwa ya kweli; alidhani alikuwa anaota ndoto.

10. Walipita kituo cha kwanza cha ulinzi na cha pili, halafu wakafika kwenye mlango wa chuma wa kuingilia mjini. Huo mlango ukawafungukia wenyewe, nao wakatoka nje. Wakawa wanatembea katika barabara moja na mara yule malaika akamwacha Petro peke yake.

11. Hapo ndipo Petro alipotambua yaliyotukia, akasema, “Sasa najua kwa hakika kwamba Bwana amemtuma malaika wake akaniokoa mikononi mwa Herode na kutoka katika mambo yale yote watu wa Israeli waliyotazamia.”

Kusoma sura kamili Matendo 12