Agano la Kale

Agano Jipya

Luka 23:34-53 Biblia Habari Njema (BHN)

34. Yesu akasema, “Baba, uwasamehe kwa maana hawajui wanalofanya.” Kisha wakagawana mavazi yake kwa kuyapigia kura.

35. Watu wakawa wamesimama pale wakitazama. Nao viongozi wakamdhihaki wakisema: “Amewaokoa wengine; sasa na ajiokoe mwenyewe, kama yeye ndiye Kristo, mteule wa Mungu!”

36. Askari nao walimdhihaki pia; walimwendea wakampa siki

37. wakisema: “Kama kweli wewe ni Mfalme wa Wayahudi, jiokoe mwenyewe.”

38. Vilevile maandishi haya yalikuwa yamewekwa juu yake: “Huyu ndiye Mfalme wa Wayahudi.”

39. Mmoja wa wale wahalifu waliotundikwa msalabani, alimtukana akisema: “Je, si kweli kwamba wewe ndiwe Kristo? Basi, jiokoe mwenyewe, utuokoe na sisi pia.”

40. Lakini yule mhalifu mwingine akamkemea mwenzake akisema: “Wewe humwogopi Mungu hata kidogo? Wewe umepata adhabu hiyohiyo.

41. Wewe na mimi tunastahili, maana haya ni malipo ya yale tuliyotenda. Lakini mtu huyu hakufanya chochote kibaya.”

42. Kisha akasema, “Ee Yesu! Unikumbuke wakati utakapoingia katika ufalme wako.”

43. Yesu akamjibu, “Nakuambia kwa hakika, leo utakuwa pamoja nami peponi.”

44. Ilikuwa yapata saa sita mchana; jua likaacha kuangaza, giza likaifunika nchi yote mpaka saa tisa,

45. na pazia lililokuwa limetundikwa hekaluni likapasuka vipande viwili.

46. Yesu akalia kwa sauti kubwa: “Baba, mikononi mwako naiweka roho yangu.” Alipokwisha sema hayo, akakata roho.

47. Hapo, yule jemadari alipoona yaliyotukia akamsifu Mungu akisema: “Hakika huyu alikuwa mtu mwema.”

48. Watu wale wote waliokuwa wamekusanyika hapo kwa ajili ya tukio hilo, walipoona hayo yaliyotukia, walirudi makwao wakijipiga vifua kwa huzuni.

49. Marafiki zake wote pamoja na wale wanawake walioandamana naye kutoka Galilaya, walisimama kwa mbali kutazama tukio hilo.

50. Kulikuwa na mtu mmoja jina lake Yosefu, mwenyeji wa kijiji kimoja cha Wayahudi kiitwacho Arimathaya. Alikuwa mtu mwema anayeheshimika.

51. Alikuwa akitazamia kuja kwa ufalme wa Mungu. Ingawa alikuwa mmoja wa Baraza Kuu la Wayahudi, hakuwa amekubaliana nao katika kitendo chao.

52. Basi, yeye alikwenda kwa Pilato, akaomba apewe mwili wa Yesu.

53. Kisha akaushusha mwili huo kutoka msalabani, akauzungushia sanda ya kitani, akauweka katika kaburi lililokuwa limechongwa kwenye mwamba, ambalo halikuwa limetumika.

Kusoma sura kamili Luka 23