Agano la Kale

Agano Jipya

1 Yohane 3:13-24 Biblia Habari Njema (BHN)

13. Basi, ndugu zangu, msishangae kama ulimwengu unawachukia nyinyi.

14. Sisi tunajua kwamba tumekwisha pita kutoka katika kifo na kuingia katika uhai kwa sababu tunawapenda ndugu zetu. Mtu asiye na upendo hubaki katika kifo.

15. Kila anayemchukia ndugu yake ni muuaji; nanyi mnajua kwamba muuaji yeyote yule hana uhai wa milele ndani yake.

16. Sisi tumepata kujua upendo ni nini, kwani Kristo aliyatoa maisha yake kwa ajili yetu. Nasi vilevile tunapaswa kuyatoa maisha yetu kwa ajili ya ndugu zetu.

17. Basi, mtu akiwa na mali za hapa duniani, halafu akamwona ndugu yake ana shida, lakini akawa na moyo mgumu bila kumwonea huruma, anawezaje kusema kwamba anampenda Mungu?

18. Watoto wangu, upendo wetu usiwe maneno matupu, bali uwe upendo wa kweli na wa vitendo.

19. Hivyo ndivyo tuwezavyo kuwa na hakika kwamba sisi ni watu wa ukweli; na hatutakuwa na wasiwasi mbele ya Mungu.

20. Kwa maana, hata kama dhamiri zetu zatuhukumu, twajua kwamba Mungu ni mkuu kuliko dhamiri, na kwamba yeye ajua kila kitu.

21. Wapenzi wangu, kama dhamiri zetu hazina lawama juu yetu, basi, twaweza kuwa na uthabiti mbele ya Mungu,

22. na kupokea kwake chochote tunachoomba, maana tunazitii amri zake na kufanya yale yanayompendeza.

23. Na, amri yake ndiyo hii: Kumwamini Mwanae Yesu Kristo, na kupendana kama alivyotuamuru.

24. Anayezitii amri za Mungu anaishi katika muungano na Mungu na Mungu anaishi katika muungano naye. Kwa njia ya Roho ambaye Mungu ametujalia, sisi twajua kwamba Mungu anaishi katika muungano nasi.

Kusoma sura kamili 1 Yohane 3