Agano la Kale

Agano Jipya

1 Wakorintho 9:17-26 Biblia Habari Njema (BHN)

17. Ningekuwa nimeichagua kazi hii kwa hiari, basi, ningetazamia malipo; lakini maadamu naifanya ikiwa ni wajibu, hiyo ina maana kwamba ni jukumu nililopewa nitekeleze.

18. Mshahara wangu ni kitu gani, basi? Mshahara wangu ni fursa ya kuihubiri Habari Njema bure, bila kudai haki ninazostahili kwa kuihubiri.

19. Kwa hiyo, ingawa mimi si mtumwa wa mtu yeyote, nimejifanya mtumwa wa kila mtu ili nimpatie Kristo watu wengi iwezekanavyo.

20. Kwa Wayahudi nimeishi kama Myahudi ili niwapate Wayahudi; yaani, ingawa mimi siko chini ya sheria, nimejiweka chini ya sheria kwao, ili niwapate hao walio chini ya sheria.

21. Na kwa wale walio nje ya sheria, naishi kama wao, nje ya sheria, ili niwapate hao walio nje ya sheria. Hii haimaanishi kwamba mimi niko nje ya sheria ya Mungu, maana nabanwa na sheria ya Kristo.

22. Kwao walio dhaifu nimejifanya dhaifu ili niwapate hao walio dhaifu. Nimejifanya kila kitu kwa wote ili nipate kuwaokoa baadhi yao kwa kila njia.

23. Nafanya haya yote kwa ajili ya Injili, nipate kushiriki baraka zake.

24. Je, hamjui kwamba katika uwanja wa michezo, ingawa wapiga mbio wote hukimbia, ni mmoja tu anayejinyakulia zawadi?

25. Wanariadha hujipa mazoezi na nidhamu kali; hufanya hivyo ili wajipatie taji iharibikayo! Lakini sisi twafanya hivyo tupate taji isiyoharibika.

26. Ndivyo basi, ninavyopiga mbio nikiwa na nia ya kushinda; ndivyo ninavyopigana, na si kama bondia anayetupa ngumi zake hewani.

Kusoma sura kamili 1 Wakorintho 9