Agano la Kale

Agano Jipya

Yoshua 7:6-19 Biblia Habari Njema (BHN)

6. Yoshua akayararua mavazi yake, yeye pamoja na wazee wa Israeli. Wakajitupa chini mbele ya sanduku la Mwenyezi-Mungu mpaka jioni; wakajitia mavumbi vichwani mwao.

7. Yoshua akasema, “Ole wetu, ee Bwana Mungu! Kwa nini umetuvusha mto Yordani ili kututia mikononi mwa Waamori watuangamize? Tungaliridhika kubaki ngambo ya mto Yordani!

8. Ee Bwana, niseme nini hali Waisraeli wamewakimbia adui zao?

9. Basi, Wakanaani pamoja na wakazi wote wa nchi hii watakapopata habari hiyo watatuzingira na kutufuta kabisa duniani. Sasa utafanya nini kuonesha ukuu wa jina lako?”

10. Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Simama! Mbona umejitupa chini hivyo?

11. Waisraeli wametenda dhambi, maana wamelivunja agano langu nililowaamuru washike; wamevichukua baadhi ya vitu vilivyowekwa wakfu viangamizwe; wameviiba na kudanganya, wakaviweka pamoja na vitu vyao.

12. Kwa hiyo Waisraeli hawawezi kuwakabili maadui zao; wanawakimbia adui zao kwa sababu wamejifanya wenyewe kuwa kitu cha kuangamizwa! Sitakuwa pamoja nao tena msipoharibu vitu vilivyomo kati yenu vilivyotolewa viangamizwe.

13. Basi, inuka uwatakase watu, waambie wajitakase na kujitayarisha kwa siku ya kesho, maana mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nasema hivi: ‘Miongoni mwenu kuna vitu vilivyotolewa viangamizwe; hamwezi kuwakabili adui zenu mpaka vitu hivyo vimeondolewa kati yenu!

14. Kwa hiyo kesho asubuhi wote mtakuja mbele yangu, kabila baada ya kabila. Kabila nitakalolichagua litakwenda mbele, ukoo baada ya ukoo. Ukoo nitakaouchagua utakwenda mbele, jamaa baada ya jamaa. Na jamaa nitakayoichagua itakwenda mbele, mtu mmojammoja.

15. Mtu yeyote atakayepatikana akiwa na vitu vilivyotolewa viangamizwe atateketezwa kwa moto, yeye pamoja na kila kitu chake maana ameliasi agano langu mimi Mwenyezi-Mungu, akatenda jambo la aibu katika Israeli.’”

16. Basi, Yoshua akaamka asubuhi na mapema, akawaleta Waisraeli wote karibu, kabila baada ya kabila; kabila la Yuda likachaguliwa.

17. Akazileta karibu koo za Yuda, ukoo baada ya ukoo; na ukoo wa Zerahi ukachaguliwa. Akazileta karibu jamaa za ukoo wa Zerahi, jamaa baada ya jamaa; na jamaa ya Zabdi ikachaguliwa.

18. Yoshua akaileta jamaa ya Zabdi karibu, nyumba baada ya nyumba; na nyumba ya Akani mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, wa kabila la Yuda, ikachaguliwa.

19. Yoshua akamwambia Akani, “Mwanangu, mtukuze Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, msifu na kisha uniambie yale uliyotenda, wala usinifiche.”

Kusoma sura kamili Yoshua 7