Agano la Kale

Agano Jipya

Yoshua 7:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Lakini Waisraeli hawakuwa waaminifu kuhusu vile vitu vilivyotolewa viangamizwe kwani Akani mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, wa kabila la Yuda, alichukua baadhi ya vitu vilivyoamriwa viteketezwe. Kwa hiyo hasira ya Mwenyezi-Mungu ikawaka dhidi ya Waisraeli.

2. Yoshua akawatuma watu kutoka Yeriko kwenda mji wa Ai, ulio karibu ya Beth-aveni, mashariki ya Betheli, akawaambia, “Nendeni mkaipeleleze nchi.” Nao wakaenda na kuupeleleza mji wa Ai.

3. Waliporudi, wakamwambia Yoshua, “Hakuna haja kupeleka watu wote kuushambulia mji wa Ai, maana wakazi wake ni wachache tu. Watu elfu mbili au tatu watatosha.”

4. Basi, watu kama elfu tatu hivi wakaenda kuushambulia mji wa Ai, lakini wakakimbizwa na wakazi wa mji huo.

5. Watu wa Ai wakawaua Waisraeli thelathini na sita na kuwafukuza wengine kutoka lango la mji mpaka Shebarimu, wakawaua kwenye mteremko. Waisraeli wakafa moyo na kulegea kama maji.

6. Yoshua akayararua mavazi yake, yeye pamoja na wazee wa Israeli. Wakajitupa chini mbele ya sanduku la Mwenyezi-Mungu mpaka jioni; wakajitia mavumbi vichwani mwao.

7. Yoshua akasema, “Ole wetu, ee Bwana Mungu! Kwa nini umetuvusha mto Yordani ili kututia mikononi mwa Waamori watuangamize? Tungaliridhika kubaki ngambo ya mto Yordani!

8. Ee Bwana, niseme nini hali Waisraeli wamewakimbia adui zao?

9. Basi, Wakanaani pamoja na wakazi wote wa nchi hii watakapopata habari hiyo watatuzingira na kutufuta kabisa duniani. Sasa utafanya nini kuonesha ukuu wa jina lako?”

10. Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua, “Simama! Mbona umejitupa chini hivyo?

11. Waisraeli wametenda dhambi, maana wamelivunja agano langu nililowaamuru washike; wamevichukua baadhi ya vitu vilivyowekwa wakfu viangamizwe; wameviiba na kudanganya, wakaviweka pamoja na vitu vyao.

12. Kwa hiyo Waisraeli hawawezi kuwakabili maadui zao; wanawakimbia adui zao kwa sababu wamejifanya wenyewe kuwa kitu cha kuangamizwa! Sitakuwa pamoja nao tena msipoharibu vitu vilivyomo kati yenu vilivyotolewa viangamizwe.

Kusoma sura kamili Yoshua 7