Agano la Kale

Agano Jipya

Yoshua 4:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Taifa zima lilipokwisha vuka mto Yordani, Mwenyezi-Mungu akamwambia Yoshua,

2. “Chagua watu kumi na wawili miongoni mwa hao Waisraeli, yaani mtu mmoja kutoka kila kabila,

3. uwaagize hivi, ‘Chukueni mawe kumi na mawili kutoka hapa katikati ya mto Yordani, kutoka hapa ilipo miguu ya makuhani, muyachukue mawe hayo, mkayaweke mahali pale ambapo mtalala leo hii.’”

4. Yoshua akawaita hao watu kumi na wawili ambao alikuwa amewateua miongoni mwa Waisraeli, kila kabila mtu mmoja,

5. akawaambia, “Litangulieni sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mpaka katikati ya mto Yordani. Kila mmoja wenu achukue jiwe begani mwake, jiwe moja kwa ajili ya kila kabila la Israeli.

6. Jambo hilo litakuwa ishara kati yenu; na watoto wenu watakapowauliza siku zijazo ‘Je, mawe haya yana maana gani kwenu?’

7. Nyinyi mtawaambia, ‘Sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu lilipopitishwa mtoni Yordani, maji ya mto huo yalizuiliwa yasitiririke!’ Kwa hiyo mawe haya yatakuwa ukumbusho kwa Waisraeli milele.”

8. Wale wanaume wakafanya kama walivyoamriwa na Yoshua, wakachukua mawe kumi na mawili kutoka katikati ya mto Yordani, jiwe moja kwa ajili ya kila kabila la Israeli, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwambia Yoshua, wakaenda nayo hadi mahali pale walipolala, wakayaweka huko.

9. Yoshua akasimika pia mawe kumi na mawili katikati ya mto Yordani, mahali pale ambapo nyayo za makuhani waliobeba lile sanduku la agano zilisimama. Mawe hayo yako huko mpaka hivi leo.

10. Wale makuhani waliobeba sanduku la agano, walisimama katikati ya mto Yordani mpaka watu walipomaliza kutekeleza kila kitu ambacho Mwenyezi-Mungu alimwamuru Yoshua awaambie watu; Yoshua alifanya yote ambayo Mose alikuwa amemwamuru. Watu wakaharakisha kuvuka mto,

11. na watu wote walipokwisha vuka, wale makuhani wakawatangulia na lile sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu.

12. Wanaume wa kabila la Reubeni na la Gadi na nusu ya kabila la Manase waliwatangulia Waisraeli wakiwa na silaha zao, kama vile walivyoagizwa na Mose.

13. Watu wapatao 40,000 wakiwa na silaha tayari kwa vita walipita mbele ya Mwenyezi-Mungu wakielekea bonde la mji wa Yeriko.

Kusoma sura kamili Yoshua 4