Agano la Kale

Agano Jipya

Yoshua 2:2-10 Biblia Habari Njema (BHN)

2. Mfalme wa mji wa Yeriko akaambiwa, “Tazama, wanaume wawili Waisraeli wameingia mjini leo usiku ili kuipeleleza nchi.”

3. Mfalme wa Yeriko akatuma watu kwa Rahabu, akisema: “Watoe nje watu waliokuja nyumbani kwako kwani wamekuja kuipeleleza nchi yote.”

4. Lakini, yule mwanamke alikuwa amekwisha waficha watu hao wawili. Basi, akawaambia wajumbe hao, “Ni kweli kwamba hao watu walikuja kwangu, lakini mimi sikujua wametoka wapi.

5. Wakati wa kufunga lango la mji, giza lilipoingia, hao watu waliondoka. Kule walikokwenda mimi sijui; wafuateni upesi nanyi mtawapata.”

6. Lakini Rahabu alikuwa amewapandisha hao wapelelezi kwenye paa na kuwaficha kwa mabua ya kitani aliyokuwa ameyatandaza huko paani.

7. Basi, wale watu waliotumwa na mfalme wakawafuatia kwa kupitia njia iliyokuwa imeelekea kwenye vivuko vya Yordani. Na mara tu walipoondoka mjini, lango la mji likafungwa.

8. Rahabu akawaendea hao wapelelezi juu darini kabla hawajalala,

9. akawaambia, “Mimi ninajua kwamba Mwenyezi-Mungu amewapa nchi hii; tumekumbwa na hofu juu yenu na wakazi wote wa nchi hii wamekufa moyo kwa sababu yenu.

10. Maana tumesikia jinsi Mwenyezi-Mungu alivyoyakausha maji ya bahari ya Shamu mbele yenu mlipotoka nchi ya Misri, na jinsi mlivyowatendea wafalme wawili wa Waamori waliokuwa ngambo ya mto Yordani, yaani Sihoni na Ogu, ambao mliwaangamiza kabisa.

Kusoma sura kamili Yoshua 2