Agano la Kale

Agano Jipya

Yoshua 11:12-21 Biblia Habari Njema (BHN)

12. Pia aliiteketeza miji ile mingine yote kwa moto na kuwaua wafalme wao wote kama Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, alivyomwamuru.

13. Lakini Waisraeli hawakuiteketeza miji iliyokuwa vilimani, isipokuwa tu mji wa Hazori ambao Yoshua aliuteketeza.

14. Waisraeli wakachukua vitu vyote walivyoteka nyara na wanyama wa miji hiyo; lakini waliwaua wakazi wake wote, wala hawakumwacha hata mtu mmoja.

15. Amri hii alipewa Mose, mtumishi wa Mwenyezi-Mungu, naye Mose akamwamuru Yoshua ambaye aliitekeleza. Yoshua alitimiza kila jambo Mwenyezi-Mungu alilomwamuru Mose.

16. Yoshua aliiteka nchi nzima: Sehemu za milimani na sehemu zote za Negebu, eneo lote la Gosheni, nchi tambarare, nchi ya Araba, milima ya Israeli na sehemu zake zilizo tambarare;

17. aliwateka na kuwaua wafalme wote wa nchi hizo kuanzia mlima uliokuwa mtupu wa Halaki karibu na Seiri mpaka Baal-gadi katika bonde la Lebanoni, kusini ya mlima Hermoni.

18. Vita alivyopigana Yoshua na wafalme hawa wote vilichukua muda mrefu.

19. Hakuna mji ambao ulifanya mapatano ya amani na Waisraeli, isipokuwa Gibeoni tu, ambamo waliishi Wahivi. Waisraeli waliiteka miji mingine yote kwa kupigana vita.

20. Ilikuwa ni matakwa ya Mwenyezi-Mungu mwenyewe kuishupaza mioyo ya watu wa mataifa hayo ili wapigane. Alikusudia wasihurumiwe ila wateketezwe. Ndivyo Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.

21. Wakati huo, Yoshua alikwenda, akawaangamiza Waanaki waliokuwa wanaishi katika milima huko Hebroni, Debiri, Anabu, nchi yote ya milima ya Yuda na Israeli. Yoshua aliwaangamiza watu hao pamoja na miji yao.

Kusoma sura kamili Yoshua 11