Sura

  1. 1
  2. 2
  3. 3
  4. 4

Agano la Kale

Agano Jipya

Yona 4 Biblia Habari Njema (BHN)

Yona anakasirika kwa sababu Mungu ana huruma

1. Lakini jambo hilo halikumpendeza Yona hata kidogo, akakasirika sana.

2. Kwa hiyo akaomba, “Mwenyezi-Mungu, je, hayo si mambo yaleyale niliyowaza utayafanya nilipokuwa nyumbani? Ndio maana nilifanya haraka kukimbilia Tarshishi. Nilijua kwamba wewe u Mungu wa upendo na huruma. Hukasiriki upesi, daima u mwema na u tayari kubadili nia yako wakati wowote ili usiadhibu.

3. Basi, sasa ee Mwenyezi-Mungu, nakusihi uniondolee uhai wangu, maana, kwangu mimi ni afadhali kufa kuliko kuishi.”

4. Naye Mwenyezi-Mungu akamjibu Yona: “Unadhani wafanya vema kukasirika?”

5. Ndipo Yona akatoka nje ya mji, akajikalia upande wa mashariki wa mji huo. Hapo, akajijengea kibanda, akaketi kivulini mwake huku anangojea apate kuona litakaloupata mji wa Ninewi.

6. Mungu, Mwenyezi-Mungu akaamuru mmea uote na kukua. Akauotesha ili kumpatia Yona kivuli cha kumpunguzia taabu aliyokuwa nayo. Yona akaufurahia sana mmea huo.

7. Lakini siku ya pili, kulipopambazuka, Mungu akaamuru mdudu auharibu mmea huo, ukanyauka.

8. Jua lilipochomoza, Mungu akaleta upepo wa hari kutoka mashariki, jua likamchoma sana Yona kichwani, karibu azirai. Yona akasema, “Afadhali kufa kuliko kuishi!”

9. Lakini Mungu akamwambia Yona, “Je, unadhani wafanya vema kuukasirikia mmea huo?” Yona akajibu, “Ndiyo, nafanya vema kukasirika – kukasirika hata kufa!”

10. Hapo Mungu akamwambia, “Mmea huu uliota na kukua kwa usiku mmoja, na usiku uliofuata ukanyauka. Wewe hukuufanyia kitu chochote, wala hukuuotesha. Mbona unauhurumia?

11. Je, haifai kwangu kuuhurumia mji wa Ninewi, ule mji mkuu wenye watu 120,000, wasioweza kupambanua jema na baya, na pia wanyama wengi?”