Agano la Kale

Agano Jipya

Yeremia 52:5-18 Biblia Habari Njema (BHN)

5. Mji uliendelea kuzingirwa mpaka mwaka wa kumi na moja wa utawala wa Sedekia.

6. Katika siku ya tisa ya mwezi wa nne, njaa ilikuwa kali sana mjini hata hapakuwa na chakula chochote kwa ajili ya wakazi wake.

7. Basi, sehemu ya ukuta wa mji ilibomolewa, nao askari walikimbia wakatoka nje ya mji wakati wa usiku wakipitia njia ya lango katikati ya kuta mbili, kwenye bustani ya mfalme, wakaenda upande wa Araba, ingawa Wakaldayo walikuwa wameuzunguka mji wote. Waisraeli walikimbia kuelekea bonde la mto Yordani.

8. Lakini jeshi la Wakaldayo lilimfuatia mfalme na kumteka katika tambarare za Yeriko, jeshi lake lote likatawanyika na kumwacha.

9. Basi Wakaldayo walimteka mfalme, wakampeleka kwa mfalme wa Babuloni, huko Ribla, katika nchi ya Hamathi, naye akamhukumu.

10. Hukohuko Ribla, mfalme wa Babuloni aliwaua wana wa Sedekia mbele ya baba yao. Aliwaua pia maofisa wote wa Yuda.

11. Kisha aliyangoa macho ya Sedekia na kumfunga pingu, akamchukua Sedekia Babuloni na kumtia kizuizini mpaka siku alipokufa.

12. Katika siku ya kumi ya mwezi wa tano, mwaka wa kumi na tisa wa utawala wa Nebukadneza, mfalme wa Babuloni, Nebuzaradani kapteni wa walinzi wa mfalme ambaye alimtumikia mfalme wa Babuloni, aliingia Yerusalemu.

13. Alichoma moto nyumba ya Mwenyezi-Mungu, ikulu na nyumba zote za Yerusalemu; kila nyumba kubwa ilichomwa moto.

14. Askari wote wa Wakaldayo waliokuwa pamoja na kapteni wa walinzi, walizibomoa kuta zote zilizouzunguka mji wa Yerusalemu.

15. Nebuzaradani kapteni wa walinzi wa mfalme, aliwachukua uhamishoni watu waliokuwa wamebakia mjini na wale waliokuwa wamejisalimisha kwa mfalme wa Babuloni pamoja na mafundi.

16. Lakini Nebuzaradani kapteni wa walinzi wa mfalme, aliwaacha baadhi ya watu waliokuwa maskini kabisa nchini, wawe watunza mizabibu na wakulima.

17. Wakaldayo walivunja vipandevipande nguzo za shaba nyeusi ambazo zilikuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu pamoja na vikalio na birika kubwa la shaba nyeusi lililokuwamo katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, wakaichukua shaba nyeusi yote mpaka Babuloni.

18. Kadhalika, walichukua vyungu, sepetu, mikasi, makarai, vijiko vikubwa na vyombo vyote vya shaba nyeusi vilivyotumiwa katika huduma ya hekalu.

Kusoma sura kamili Yeremia 52