Agano la Kale

Agano Jipya

Yeremia 44:3-13 Biblia Habari Njema (BHN)

3. Imekuwa hivyo kwa sababu ya uovu walioufanya, wakanikasirisha kwa kuifukizia ubani na kuitumikia miungu mingine ambayo wao wenyewe hawakuifahamu, wala nyinyi, wala wazee wenu.

4. Hata hivyo, mimi daima niliwatuma kwenu watumishi wangu manabii nikisema: Msifanye jambo hili baya ninalolichukia!

5. Lakini hakuna aliyenisikiliza wala kunitegea sikio. Nyinyi mlikataa kuacha uovu wenu na kuacha kuifukizia ubani miungu mingine.

6. Kwa hiyo, ghadhabu yangu na hasira yangu iliwaka na kumiminika juu ya miji ya Yuda na barabara za Yerusalemu, hata kukawa jangwa na magofu kama ilivyo mpaka leo.

7. “Sasa, mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, nauliza hivi: Mbona mnajiletea madhara makubwa namna hii, na kujiangamiza nyinyi wenyewe, wanaume kwa wanawake, watoto wadogo na wachanga, hata pasibaki mtu katika Yuda?

8. Kwa nini mnanichochea nikasirike kwa kuabudu sanamu mlizojitengenezea wenyewe na kuifukizia ubani miungu mingine katika nchi ya Misri ambamo mmekuja kuishi? Je, mwataka kutokomezwa na kuwa laana na dhihaka mbele ya mataifa yote duniani?

9. Je, mmesahau uovu wa wazee wenu, uovu wa wafalme wa Yuda, uovu wa wake zao na uovu wenu nyinyi wenyewe na wa wake zenu, ambao mliufanya nchini Yuda na kwenye barabara za Yerusalemu?

10. Mpaka hivi leo hamjajinyenyekesha wala kuogopa wala kuzifuata sheria zangu na kanuni zangu nilizowawekea nyinyi na wazee wenu.

11. “Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, nasema hivi: Haya! Nitawageukia niwaleteeni maafa na kuiangamiza Yuda yote.

12. Nitawaondoa watu wa Yuda waliosalia ambao wamepania kwenda kukaa Misri, na kuwaangamiza wote, wakubwa kwa wadogo; watakufa kwa upanga au kwa njaa. Watakuwa takataka, kitisho, laana na dhihaka.

13. Nitawaadhibu wale wanaokaa katika nchi ya Misri kama nilivyouadhibu mji wa Yerusalemu, kwa vita, njaa, na maradhi mabaya.

Kusoma sura kamili Yeremia 44