Agano la Kale

Agano Jipya

Yeremia 36:2-13 Biblia Habari Njema (BHN)

2. “Chukua kitabu uandike humo maneno yote niliyokuambia juu ya Israeli, juu ya Yuda na mataifa yote, tangu siku nilipoanza kuongea nawe, wakati Yosia alipokuwa mfalme mpaka leo.

3. Labda watu wa Yuda watasikia juu ya maovu yote ambayo nimenuia kuwatendea, ili kila mmoja wao auache mwenendo wake mbaya, nami nipate kuwasamehe makosa yao na dhambi yao.”

4. Ndipo Yeremia akamwita Baruku mwana wa Neria. Naye Baruku akaandika katika kitabu maneno yote aliyotamka Yeremia ambayo Mwenyezi-Mungu alikuwa amemwambia.

5. Kisha, Yeremia akampa Baruku maagizo yafuatayo: “Mimi siruhusiwi kwenda katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu.

6. Lakini mnamo siku ya kwanza ya mfungo, wewe utakwenda mbele ya umati wote wa watu, ndani ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, usome hati ndefu ya maneno ya Mwenyezi-Mungu niliyokuamuru uandike kama nilivyoyasema. Utayasoma maneno hayo pia mbele ya watu wote wa Yuda waliofika kutoka miji yao.

7. Labda maombi yao yatamfikia Mwenyezi-Mungu na kwamba kila mmoja wao ataacha mwenendo wake mwovu kwa maana Mwenyezi-Mungu ametamka adhabu dhidi ya watu hawa kwa hasira na ghadhabu kali.”

8. Basi, Baruku mwana wa Neria, alitimiza yote aliyoamriwa na nabii Yeremia kuhusu kusoma maneno ya Mwenyezi-Mungu ndani ya nyumba yake Mwenyezi-Mungu kutoka katika kitabu hicho.

9. Mnamo mwaka wa tano wa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, katika mwezi wa tisa, wakazi wote wa Yerusalemu na watu wote waliofika Yerusalemu kutoka miji ya Yuda, walitangaza siku ya mfungo mbele ya Mwenyezi-Mungu.

10. Basi, Baruku alisoma maneno ya Yeremia kutoka katika kile kitabu mbele ya watu wote, ndani ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu, katika chumba cha Gemaria mwana wa Shafani aliyekuwa katibu. Chumba hicho kilikuwa katika ukumbi wa juu, kwenye lango Jipya la nyumba ya Mwenyezi-Mungu.

11. Mikaia mwana wa Gemaria, mwana wa Shafani, aliposikia maneno yote ya Mwenyezi-Mungu ambayo yalisomwa kutoka kile kitabu,

12. alikwenda ikulu kwa mfalme katika chumba cha katibu walimokuwa wameketi wakuu wote: Katibu Elishama, Delaya mwana wa Shemaya, Elnathani mwana wa Akbori, Gemaria mwana wa Shafani, Sedekia mwana wa Hanania, na wakuu wote.

13. Mikaia aliwaambia maneno yote aliyoyasikia wakati Baruku aliposoma kitabu mbele ya umati wa watu.

Kusoma sura kamili Yeremia 36