Agano la Kale

Agano Jipya

Yeremia 34:1-11 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Yeremia wakati Nebukadneza, mfalme wa Babuloni, pamoja na jeshi lake lote na falme zote za dunia zilizokuwa chini yake, kadhalika na watu wote walipokuwa wakiushambulia mji wa Yerusalemu na miji mingine yote ya kandokando yake:

2. “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli asema hivi: Nenda ukaongee na Sedekia, mfalme wa Yuda. Mwambie kwamba mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nimeutia mji huu mikononi mwa mfalme wa Babuloni, naye atauteketeza kwa moto.

3. Nawe hutatoroka mikononi mwake, bali kwa hakika utatekwa na kupelekwa kwake; utaonana na mfalme wa Babuloni macho kwa macho, na kuongea naye ana kwa ana; kisha, utakwenda Babuloni.

4. Lakini, ewe Sedekia, mfalme wa Yuda, mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi juu yako: Wewe hutauawa kwa upanga vitani.

5. Utakufa kwa amani. Na, kama vile watu walivyochoma ubani walipowazika wazee wako waliokuwa wafalme, ndivyo watakavyokuchomea ubani na kuomboleza wakisema, ‘Maskini! Mfalme wetu amefariki!’ Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”

6. Kisha, nabii Yeremia akamweleza Sedekia, mfalme wa Yuda, maneno hayo yote huko Yerusalemu,

7. wakati jeshi la mfalme wa Babuloni lilipokuwa linaushambulia mji wa Yerusalemu na pia miji ya Lakishi na Azeka, ambayo ilikuwa miji pekee iliyosalia yenye ngome.

8. Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Mwenyezi-Mungu baada ya mfalme Sedekia kufanya agano na watu wote wa Yerusalemu kuwaachia huru

9. watumwa wao wa Kiebrania wa kiume na wa kike, ili mtu yeyote asimfanye Myahudi mwenzake mtumwa.

10. Viongozi wote na watu wote waliofanya agano hilo walikubaliana wote wawaachie huru watumwa wao wa kiume na wa kike, na mtu yeyote asiwafanye tena kuwa watumwa. Walikubaliana, wakawaacha huru.

11. Lakini baadaye walibadili nia zao, wakawashika tena watumwa hao wa kiume na wa kike ambao walikuwa wamewaacha huru, wakawafanya watumwa.

Kusoma sura kamili Yeremia 34