Agano la Kale

Agano Jipya

Yeremia 33:15-26 Biblia Habari Njema (BHN)

15. Katika siku hizo, naam, wakati huo, nitachipusha chipukizi mwadilifu wa uzao wa Daudi. Chipukizi huyo atatekeleza haki na uadilifu katika nchi.

16. Wakati huo nchi ya Yuda itaokolewa na mji wa Yerusalemu utakuwa salama. Na mji huo utaitwa ‘Mwenyezi-Mungu ni Ukombozi Wetu’.

17. Maana mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Hapatakosekana kamwe mzawa wa Daudi atakayetawala Israeli.

18. Kadhalika nao makuhani wa ukoo wa Lawi watakuwapo daima kunihudumia wakinitolea sadaka za kuteketezwa na sadaka za nafaka na kunitolea tambiko milele.”

19. Neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Yeremia:

20. “Kama vile hamwezi kutangua agano langu nililoweka kuhusu usiku na mchana hivyo kwamba usiku na mchana visiweko kama nilivyopanga,

21. vivyo hivyo hamwezi kutangua agano langu nililofanya na mtumishi wangu Daudi. Nilifanya agano na Daudi kwamba daima atakuwa na mzawa wa kutawala mahali pake; vilevile kutakuwako daima makuhani wa ukoo wa Lawi watakaonitumikia.

22. Kama vile nyota angani na mchanga wa pwani visivyohesabika, ndivyo nitakavyoongeza idadi ya wazawa wa mtumishi wangu Daudi na idadi ya makuhani wa ukoo wa Lawi.”

23. Neno la Mwenyezi-Mungu lilimjia Yeremia:

24. “Je, hujasikia wasemayo watu hawa, kwamba mimi Mwenyezi-Mungu nimewatupilia mbali watu wa Israeli na watu wa Yuda, jamaa mbili nilizoziteua? Wamewadharau watu wangu, hata kuwaona kwamba wao si taifa.

25. Lakini mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Mimi niliweka agano kuhusu mchana na usiku na kuweka sheria za mbingu na dunia.

26. Basi, ndivyo ilivyo pia: Sitawatupa wazawa wa Yakobo na Daudi, mtumishi wangu; nitamteua mmoja wa wazawa wake atawale wazawa wa Abrahamu, Isaka na Yakobo. Kwa maana nitawarudishia fanaka yao na kuwahurumia.”

Kusoma sura kamili Yeremia 33